Uhalifu wa Kivita: Jengo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran lalengwa katika hujuma ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i127614
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali shambulizi la kigaidi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya moja ya majengo yake katika mji mkuu, Tehran.
(last modified 2025-06-16T07:47:54+00:00 )
Jun 16, 2025 07:47 UTC
  • Uhalifu wa Kivita: Jengo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran lalengwa katika hujuma ya Israel

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali shambulizi la kigaidi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya moja ya majengo yake katika mji mkuu, Tehran.

Kwa mujibu wa taarifa shambulizi hilo dhidi ya Taasisi ya Mafunzo ya Siasa na Kimataifa (IPIS) limepelekea kujeruhiwa watu wengi wakiwemo wafanyakazi wa wizara.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Saeed Khatibzadeh, katika taarifa yake Jumapili, alikemea shambulio hilo kama kitendo "cha makusudi na cha kikatili" kilichotekelezwa na "utawala katili wa Israel."

Khatibzadeh ambaye pia ni msimamizi wa taasisi hiyo amesema: "Waliojeruhiwa ni pamoja na baadhi ya wafanyakazi wenzangu, ambao walihamishiwa hospitalini kwa ajili ya matibabu."

Khatibzadeh amelitaja tukio hilo kama "uhalifu mwingine wa kivita usio na aibu." Aidha amesema ni sehemu ya "uchokozi unaoendelea na wa kimfumo" wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Wakati huo huo msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Esmail Baghaei, amesema Israel inahadaa inaposema kuwa inatekeleza " "mashambulizi kwa umakini, bila uharibifu wa makazi."

Katika ujumbe wake kwenye X, zamani Twitter, Baghaei ameashiria mashambulizi ya karibuni ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya maeneo ya raia katika mji mkuu, Tehran, ambayo kimsingi yanalenga watoto na wanawake wasio na hatia.

Amesema:  "Katika mashambulizi matatu ya hivi karibuni yaliyotekelezwa na Israel jijini  Tehran, wanawake na watoto 73 wameuawa." Baghaei ameongeza kuwa "Watoto 20 waliouawa katika mtaa wa Chamran, 10 bado wamekwama chini ya vifusi."

Moja ya mashambulizi mabaya zaidi ya Israeli katika saa za alfajiri ya Ijumaa asubuhi yalilenga jengo la makazi katika kitongoji cha Nobonyad kaskazini mwa Tehran, na kuua raia 60, wakiwemo watoto 20.

Kulingana na taarifa kutoka Wizara ya Afya ya Iran, jumla ya watu 224 wameuawa katika mawimbi mengi ya mashambulizi ya anga ya Israel, yaliyoanza Juni 13 ambayo yanatekelezwa kwa msaada wa Marekani.

Waziri wa Afya wa Iran, Dakta Mohammadreza Zafarghandi, pia amesema wengi wa waathirika wa uchokozi wa Israel nchini Iran katika siku za hivi karibuni wamekuwa raia, ikiwemo idadi kubwa ya wanawake na watoto.