Rais wa Iran: Ni lazima tuungane dhidi ya uchokozi wa utawala wa kijinai wa Israel
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesema wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu wanahitaji umoja na mshikamano wakati huu kuliko wakati mwingine wowote ule, na lazima washikane mikono na kusimama kidete kukabiliana na uchokozi wa utawala wa Israel unaofanya mauaji ya kimbari.
Rais Pezeshkian ameyasema hayo leo Jumatatu katika kikao cha Bunge ambapo amelaani hujuma za jinai za utawala ghasibu wa Israel katika mauaji ya makamanda wa kijeshi na wanasayansi wa nyuklia wa Iran pamoja na makumi ya raia.
“Adui hawezi kutuondoa sisi au taifa letu kwenye tukio kupitia jinai, mauaji, na mauaji ya kigaidi,” Pezeshkian amesema na kuongeza, “Kwa kila shujaa anayeuawa shahidi, mamia zaidi watasimama ili kubeba bendera na kusimama dhidi ya ukandamizaji, dhulma, uhalifu, na usaliti unaofanywa na wavamizi hao.”
"Hivi ndivyo watu wetu wameonyesha mara kwa mara - kusimama imara katika kukabiliana na ukatili kama huo," amesema Rais wa Iran ambaye pia ametoa wito wa umoja wa kitaifa, akisisitiza kuwa Iran haikuanzisha vita hivi.
Ameeleza bayana kuwa, "Leo, kuliko wakati mwingine wowote, tunahitaji umoja na mshikamano. Wairani wote lazima waungane na kusimama kidete kupinga kitendo hiki cha uchokozi. Tofauti zozote au matatizo yaliyopo lazima yawekwe kando sasa. Ni lazima tuungane na kukabiliana kwa uthabiti na uchokozi huu wa uhalifu wa mauaji ya halaiki."
Dakta Pezeshkian amesema kuwa, Iran ina haki ya kunufaika na nishati ya nyuklia na utafiti unaohudumia maslahi ya taifa, na akaongeza kuwa hakuna mtu ana haki ya kuinyima haki hii Jamhuri ya Kiislamu. "Tunasimama kidete katika kufikia haki hii na hatuogopi nguzu zozote katika kupata kile ambacho ni haki yetu. Tumenyoosha mkono wa udugu kwa mataifa yote ya Kiislamu - kwani wote ni ndugu zetu. Leo, wengi, ikiwa sio wote, wanasimama nasi na upande wetu," ameongeza Rais wa Iran.

Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf amesema Jeshi la Iran litamuacha adui "mshenzi" wa Israel katika hali mbaya, kwani utawala huo haujali mstari wowote mwekundu.
Akizungumza katika kikao cha wazi cha Bunge leo Jumatatu, Ghalibaf amesema jinamizi lililoshuhudiwa na Wazayuni katika nyusiku zilizopita na hofu kubwa ya watendani na wachochezi wa jinai za utawala wa Kizayuni, litaendelea hadi mvamizi apate majuto kwa adhabu itakayomsibu. Ameongeza kuwa, majeshi ya Iran yatawatia maadui kwenye Jahannamu, na walimwengu watashuhudia masaibu yao.