Rais wa Iran: Hatukuanzisha vita sisi, lakini tutatoa jibu kali kwa uvamizi wa Israel
(last modified Sun, 22 Jun 2025 15:13:24 GMT )
Jun 22, 2025 15:13 UTC
  • Rais wa Iran: Hatukuanzisha vita sisi, lakini tutatoa jibu kali kwa uvamizi wa Israel

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Iran haikuanzisha vita lakini itatoa jibu kali kwa uvamizi wa utawala haramu wa Israel dhidi yake.

Daktari Pezeshkian amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Rais wa Misri, Abdel-Fattah al-Sisi na kubainisha kwamba, "Sisi hatukuanzisha vita wala hatuna nia ya kuviendelezaa, lakini jibu letu kwa kuendelea kwa uchokozi ni kali."

Sambamba na kusifu misimamo imara, yenye maamuzi na ya kindugu ya Rais wa Misri na nchi yake kuhusiana na uvamizi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi Iran, amesema: "Tangu mwanzo nimekuwa na ninaendelea kutafuta maridhiano ndani ya Iran na maingiliano na walimwengu, hususan nchi jirani na za Kiislamu ambazo tuna uhusiano mkubwa nazo."

Akigusia shambulio la utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran wakati wa mazungumzo na Marekani, Rais Pezeshkian ameongeza kuwa: "Tulikuwa tukitafuta kutatua masuala kwa njia ya mazungumzo, lakini utawala wa Kizayuni ulivamia ardhi yetu; hatukuanzisha vita hivyo, wala hatuna nia ya kuendeleza vita hivyo, lakini iwapo uchokozi huo utaendelea, tutatoa jibu madhubuti."

Kwa upande wake, Rais wa Misri kwa mara nyingine tena almelaani vikali hujuma ya Israel dhidi ya Iran na kusema: "Tunashauriana na pande mbalimbali, ikiwemo Marekani, ili kutuliza mivutano na kusimamisha vita, na tunasisitiza kuwa ni lazima kufunguliwe nafasi kwa mashauriano ya kidiplomasia."