Umuhimu wa vikao na mashauriano aliyofanya Rais wa Iran katika mkutano wa ECO
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambaye alikuweko nchini Jamhuri ya Azerbaijan alikohudhuria mkutano wa Jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi, ECO, alikutana na viongozi wa nchi zingine wanachama wa jumuiya hiyo, wakabadilishana Mawazo kuhusu matukio ya kikanda na namna ya kupanua ushirikiano kati ya pande mbili.
Akiizungumzia safari yake hiyo ya siku moja katika Jamhuri ya Azerbaijan sambamba na kuashiria anga ya kikao kikuu cha mkutano wa ECO, Rais Pezeshkian amesema, nchi zote zilizohudhuria mkutano huo zililaani kwa msisitizo na kwa sauti moja vitendo vya kijinai vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran. Baada ya kurejea kutoka safari hiyo, Pezeshkian alizungumzia vikao vya baina ya mbili alivyofanya kando ya mkutano wa ECO na akasema: "tulifanya vikao vizuri sana vya kujenga na viongozi wa nchi wanachama wa ECO, ambapo tulijadili kuhusu namna ya kuendeleza uratibu, na kuimarisha maingiliano ya kidiplomasia na mashirikiano ya pamoja ya kiuchumi.
Rais wa Iran ameashiria pia mazungumzo ya baina ya pande mbili aliyofanya na Rais Recep Tayyib Erdogan wa Uturuki na Ilham Aliyev wa Jamhuri ya Azerbaijan na akasema: "mazungumzo na Rais wa Uturuki yalikuwa chanya na tulizungumzia masuala ya kiuchumi na vilevile uchokozi uliofanywa na utawala wa Kizayuni. Rais wa Uturuki alilaani kwa uwazi kabisa uchokozi wa utawala huo na tukabadilishana mawazo kuhusu uratibu wa kidiplomasia katika siku za usoni. Pezeshkian ameongeza kuwa, mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Azerbaijan nayo pia yalifanyika katika anga chanya na ya kirafiki, na yalipatikana matunda mazuri kuhusiana na kuwepo maingiliano ya kiuchumi na kikanda.
Huku akisisitiza kuwa safari na maingiliano hayo yanaweza kuandaa mazingira ya kuimarisha uhusiano na nchi za Kiislamu, Rais Pezeshkian amesema: "inapasa viongozi na maafisa watendaji wa nchi husika wachukue hatua za kivitendo zaidi katika nyuga za sayansi, uchukuzi, utamaduni na uendeshaji wa warsha. Rais wa Iran ametuma salamu maalumu pia akisisitiza kwa kusema: kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ECO ni nembo kubwa ya diplomasia ya ujirani na inaongoza katika diplomasia ya kiuchumi ya baina ya pande kadhaa.
Siku ya Ijumaa ya tarehe 4 Julai, Dkt Pezeshkian alifanya safari ya siku moja ya kuhudhuria kikao cha 17 cha viongozi wa nchi wanachama wa ECO kilichofanyika mjini Khankendi kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Azerbaijan ambako mbali na kukutana na kufanya mazungumzo na marais wa Azerbaijan na Uturuki, alionana na kubadilishana mawazo pia na Waziri Mkuu wa Pakistan Shahbaz Sharif na Rais Emomali Rahmon wa Tajikistan. Alipohutubia mkutano wa ECO, Rais Pezeshkian aliashiria hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Iran na akasema: kwa mujibu wa Ibara ya 51 ya Hati ya Umoja wa Mataifa, vikosi vya ulinzi vya Iran vilichukua hatua ya kuwahami kisheria wananchi wa Iran, mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi yote ya nchi na vikatoa funzo kubwa kwa wavamizi na kuzuia kuenea vita katika eneo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliongezea kwa kusema: ninatoa shukurani kwa misimamo ya uwajibikaji ya nchi za eneo na wanachama wa jumuiya ya ECO katika muda wote wa mgogoro. Jumuiya nyingi za kimataifa na kikanda kikiwemo kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Kiislamu zilichukua msimamo thabiti wa kulaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran.ECO ni jumuiya muhimu ya kiuchumi inayojumuisha nchi 8 wanachama, ikiwa ni pamoja na Iran, Uturuki, Pakistan na Jamhuri ya Azerbaijan, lengo lake likiwa ni kustawisha biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi. Kuhudhuria Rais Pezeshkian mkutano wa ECO kunadhihirisha dhamira ya Iran ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi katika eneo. Aidha, kwa kuzingatia ushiriki wa viongozi wa ngazi za juu wa nchi nyingine katika mkutano huo, safari hiyo ya rais wa Iran inadhihirisha umuhimu ambao Jamhuri ya Kiislamu imeupa mkutano wa Khankendi na uhusiano wake na wanachama wa ECO.
Iran ina mchango na nafasi muhimu sana katika njia za upitishaji bidhaa za Kaskazini-Kusini na Mashariki-Magharibi, na kuhudhuria kwakea mkutano huo kunaweza kusaidia uendelezaji wa miradi ya pamoja kama vile reli ya Rasht-Astara na miradi mingine ya miundombinu. Kuwa mwenyeji Baku wa mkutano huo, nako pia kulitoa fursa ya kufanya mazungumzo ya pembeni na maafisa wa Jamhuri ya Azerbaijan.
Kuhudhuria Rais Pezeshkian mkutano wa wakuu wa ECO kulikuwa na umuhimu kiuchumi katika biashara, upitishaji wa bidhaa na uwekezaji na pia kisiasa katika kuimarisha diplomasia na uhusiano wa pande mbili; na kunadhihirisha juhudi zinazofanywa na Iran za kutoa mchango mkubwa na athirifu zaidi katika ushirikiano wa kikanda. Sambamba na hayo, kulaaniwa vitendo vya kichokozi na kivamizi vilivyofanywa hivi karibuni na utawala wa Kizayuni katika mkutano huo kumeonyesha pia mshikamano wa nchi wanachama wa ECO na nchi jirani kwa Iran; na mshikamano huo unaweza kuandaa mazingira ya kustawishwa zaidi uhusiano kati ya nchi wanachama…/