Rais wa Iran: Uchokozi wowote utakaorudiwa utakabiliwa na jibu kali zaidi na la kujutisha zaidi
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonya kuwa, uchokozi wowote utakaorudiwa kufanywa dhidi ya ardhi ya Iran utakabiliwa na jibu kali zaidi na la kujutisha zaidi.
Rais Pezeshkian ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Rais wa Baraza la Ulaya, Antonio Costa ambayo yalijikita katika kujadili matukio ya hivi punde ya kimataifa, hususan kuhusu vita vya kulazimishwa vya siku 12 dhidi ya Iran, na matarajio yaliyopo ya uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya.
Katika mazungumzo hayo, Rais wa Iran ameashiria vitendo vya jinai vya utawala wa Kizayuni na nafasi yake haribifu katika kuvuruga amani na usalama wa dunia na akasema: nchi yetu ilivamiwa na utawala wa Kizayuni na Marekani katika hali ambayo ilikuwa kwenye njia ya majadiliano na mazungumzo, na ni wakati walipokabiliwa na jibu kali la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ndipo wakalazimika kuomba usitishaji vita. Na bila shaka utawala wa Kizayuni haungeweza Kktenda jinai hiyo bila ya uratibu na ruhusa ya Marekani.
Katika kujibu wasi wasi wa Rais wa Baraza la Ulaya kuhusu kusimamishwa ushirikiano wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaheshimu na kushikamana na misingi ya mazungumzo, diplomasia, kuheshimiana na kufuata mfumo wa sheria za kimataifa, na akauelezea mswada wa hivi karibuni wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) kuwa ni mjibizo kwa mienendo ya upendeleo na isiyoendana na utaalamu ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.
Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Ulaya ameashiria nia ya Umoja huo ya kutumia suluhisho la kidiplomasia kwa ajili ya kutatua masuala yaliyopo na kupanua ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasema: "ninakubaliana kikamilifu na wewe Mheshimiwa Rais kwamba asasi za kimataifa zinapaswa kuepuka misimamo ya kindumakuwili. Umoja wa Ulaya unaheshimu sana historia, ustaarabu na utamaduni wa taifa la Iran na uko tayari kikamilifu kwa mazungumzo na ushirikiano"…/