Iran: Itibari ya Troika ya Ulaya imeporomoka kwa kuunga mkono uvamizi wa Israel
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya sheria na kimataifa amesema kuwa Troika ya Ulaya, yaani Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zilisambaratisha itibari na uaminifu wao wenyewe kwa kuunga mkono vitendo vya uchokozi vya utawala wa Israel dhidi ya Iran.
Akizungumza katika mahojiano ya televisheni jana Jumapili, Kazem Gharibabadi amesema baadhi ya nchi ziliunga mkono utawala wa Israel wakati wa vita vyake vya kichokozi vya siku 12 dhidi ya Iran, hususan nchi tatu za Ulaya ambazo ni Uingereza, Ujerumani na Ufaransa.
"Kando na nchi hizi tatu, sikuona nchi nyingine yoyote ambayo inaunga mkono utawala wa Kizayuni, na bila shaka, Marekani, ambayo ilikuwa sehemu ya uchokozi huu," amesisitiza. Amebainisha kuwa, nchi tatu hizo za Ulaya zilihalalisha uungaji mkono wao kwa utawala wa Tel Aviv kwa kutumia "hoja zisizo na msingi."
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ameeleza kuwa, wawakilishi wa Marekani na Israel wameandaa na kuwasilisha barua kwa Umoja wa Mataifa ili kuhalalisha uchokozi huo dhidi ya Iran na kuongeza kuwa, "nchi hizo tatu pia zimekariri visingizio hivyo hivyo."
Marekani na utawala wa Israel zilidai kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ni tishio lililo karibu na ulikuwa unaelekea kwenye harakati za kijeshi, ameeleza Gharibabadi. Kwa hiyo, ameongeza, Iran ilikuwa na haki halali ya kujilinda ili kufifisha njama hizo za Marekani na Israel.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya sheria na kimataifa amesema Iran haijapokea waraka rasmi kuhusu uamilishwaji wa mfumo wa kuhuisha vikwazo dhidi ya taifa hili (snapback).
Gharibabadi amesema Iran bado haijapokea taarifa rasmi kwamba Umoja wa Ulaya unanuia kufufua utaratibu huo wa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran, lakini wanatarajia kufanya hivyo siku moja.