Kwa nini uwepo wa Araqchi katika Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ni muhimu?
Seyyed Abbas Araqchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameondoka Tehran kuelekea China akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa Tehran kwa ajili ya kuhudhuria kikao cha Mawaziri wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.
Katika safari hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran atashiriki na kutoa hotuba katika Mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, na pia kufanya mazungumzo na kubadilishana mawazo na Waziri wa Mambo ya Nje wa China na mawaziri wengine wa mambo ya nje wa nchi zinazoshiriki katika mkutano huo.
Kuhusu safari hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: 'Suala la hujuma ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran na mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya nchi yetu ni miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa katika kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.
Kuhusu kushiriki katika mkutano wa 25 wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai katika mji mkuu wa Tianjin nchini China, Araqchi ameongeza kuwa: "Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai inabadilika hatua kwa hatua kutoka jumuiya ya kieneo na kuwa ya kimataifa ambapo inajadili masuala mbalimbali katika ajenda yake, yakiwemo masuala ya kiuchumi, kisiasa na kiusalama."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa: 'Jumuiya hii ilianza shughuli zake kwa majadiliano ya kiusalama na jinsi ya kukabiliana na ugaidi, na tangu wakati huo imepanuka na kujumuisha mashauriano kuhusu biashara, Akili Mnemba, uchumi wa kidijitali, nishati na ushirikiano katika sekta hizo.' Araqchi pia ameelezea ushiriki wake katika mkutano huo kuwa ni fursa ya kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya kimataifa na matukio ya sasa ulimwenguni.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubaliwa kuwa mwanachama wa kudumu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai mwaka 2021. Kuwepo kwa Araqchi katika mkutano huu kunadhihirisha dhamira ya Iran katika ushirikiano wa pande nyingi ndani ya mfumo wa jumuiya hii na wakati huo huo kuimarisha nafasi yake kama mhusika mkuu barani Asia na katika eneo la Asia Magharibi.
Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ina jukumu muhimu katika ushirikiano wa kiusalama, kukabiliana na ugaidi na misimamo mikali pamoja na ushirikiano wa kiuchumi. Kuwepo kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika mkutano huu kunaweza kusaidia zaidi kuratibu usalama wa eneo na kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja vya Magharibi.
Kando ya mkutano huo, Araqchi atakutana na maafisa kutoka nchi wanachama zikiwemo Russia, China, Pakistan na India. Mazungumzo haya yanaweza kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kisiasa kati ya pande hizo. Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ni moja ya taasisi muhimu za kuimarisha ulimwengu wenye pande nyingi katika kukabiliana na ubeberu na udhibiti wa nchi za Magharibi.
Marekani na waitifaki wake kama vile utawala wa Kizayuni daima zimekuwa zikijaribu kutoa mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi dhidi ya nchi huru kama Iran. Ushirikiano na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai bila shaka unaziweka nchi huru kama China na Russia upande wa Iran. Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai inaweza kutetea misimamo ya Iran katika majukwaa ya kimataifa na hivyo kuzuia hatua za upande mmoja dhidi ya Tehran.
Marekani na utawala wa Kizayuni zimevuruga kabisa amani na usalama katika eneo la Asia Magharibi kupitia sera zao za uchokozi dhidi ya mataifa mengine. Kufungamana kwa Iran na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai kunaweza kusaidia kuunda anga ya uwiano wa nguvu na kupunguza ushawishi haribifu wa mhimili wa Marekani na utawala wa Kizayuni katika eneo. Ushirikiano huu sio tu kwamba utaimarisha usalama wa taifa la Iran, bali pia utapelekea kuanzishwa kwa mfumo wa pande nyingi kimataifa na hivyo kupunguza ubabe wa utawala wa Marekani na washirika wake ulimwenguni.
Kuhudhuria Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai pia kuna lengo la kupanua ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi kati ya nchi huru ili kukabiliana na kushadidi mitazamo haribifu ya Marekani na washirika wake wa Magharibi katika pembe tofauti za dunia.