Araqchi katika mkutano wa Shanghai: Israel na Marekani zilifanya jinai za kivita dhidi ya Iran
Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mkutano kikao cha Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai nchini China kwamba, utawala ghasibu wa Israel na Marekani zilifanya jinai za kivita dhidi ya Iran.
Araqchi ameyataja mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel na Marekani dhidi ya Iran kuwa ni uhalifu wa kivita na ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na akataka jamii ya kimataifa ionyeshe radiamali.
Katika hotuba yake, Araqchi ameashiria vita vya siku 12 na hujuma za wazi za Israel na Marekani dhidi ya Iran na kusema: "Kulenga zaidi ya watu 6,850 waliouawa na kujeruhiwa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kushambulia vituo vya nyuklia vya amani ni ukiukaji wa NPT na maazimio ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki." Pia, mauaji ya makamanda na wanasayansi: Idadi ya maafisa wa kijeshi na kisayansi wa Iran walilengwa majumbani mwao.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai kutoa uungaji mkono wa kisiasa na kisheria kwa Iran dhidi ya uchokozi huo, kuunda mifumo mipya ya kukabiliana na ugaidi wa nchi, vikwazo vya upande mmoja na vita vya vyombo vya habari, na kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi ili kukabiliana na vitisho vya pamoja.
Araghchi ameonya kuwa usalama katika Asia Magharibi hautapatikana maadamu Israel ina kinga. Pia alisifu jukumu la Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai katika kuunda mpangilio wa ulimwengu wa pande nyingi.