Kwa nini uwezo tofauti wa Iran unatoa fursa ya kipekee kwa maendeleo ya nchi za Kiafrika?
Katika hali ambayo nchi nyingi za Kiafrika zinakabiliwa na changamoto za miundombinu na ukosefu wa teknolojia mpya, Iran imetoa fursa mpya za ushirikiano na ubadilishanaji wa teknolojia kwa kutegemea uwezo wake wa kiufundi, kiuhandisi na kitaalamu.
Gholamreza Nouri Qazaljeh, Waziri wa Jihadi ya Kilimo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika Kamisheni ya 7 ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Kenya iliyofanyika karibuni Nairobi, mji mkuu wa Kenya kwamba: 'Tuna nia ya kuimarisha ushirikiano wetu na kuhamishia ujuzi wetu wa kiufundi katika nyanja mbalimbali nchini Kenya.
Nouri Qazaljeh ameongeza kuwa: Kustawisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Kenya ni ajenda ya tume ya pamoja ya nchi mbili, na lengo la pande zote mbili ni kufikia biashara ya dola bilioni moja.
Waziri wa Jihadi ya Kilimo wa Iran pia amesema: Kuundwa kwa kamati ya pamoja ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na Kenya kwa ajili ya kufuatilia maelewano na hati zilizotiwa saini, kufanya maonyesho ya pamoja, kuimarisha ushirikiano wa kibenki na kuondoa vikwazo vilivyopo, mipango ya muda mrefu ya kuigeuza Iran kuwa daraja linalounganisha Kenya na Caucasus na Asia ya Kati, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi kati ya nchi hizi mbili, ni miongoni mwa masuluhisho mengine yanayochunguzwa.
Tume ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Iran na Kenya inaongozwa na Waziri wa Jihad ya Kilimo wa Iran na Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi.
Mkuu huyo wa Mawaziri wa Kenya pia amesema katika mkutano huo: 'Tumekubaliana kuunda kamati ya pamoja kati ya Iran na Kenya. Tunawahimiza wafanyabiashara na wajasiriamali wa Kenya kufaidika na uwezo mkubwa wa Iran. Tume ya pamoja ya ushirikiano wa nchi hizi mbili inaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha maingiliano na maendeleo ya ushirikiano wa pande mbili.
Iran ina uwezo mkubwa anuai wa kiuchumi ambao unaweza kuwa na manufaa makubwa kwa nchi za Kiafrika. Uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa katika nyanja za ujenzi wa barabara, nyumba, miundomsingi, mafuta, gesi na bidhaa za petroli ni moja ya uwezo huu. Thamani ya soko la huduma za kiufundi na uhandisi barani Afrika inakadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 1,000, ambapo Iran inaweza kuwa na nafasi muhimu katika uwanja huo. Bidhaa za Iran kama vile dawa, vifaa vya matibabu, mitambo ya viwandani, bidhaa za petrokemikali na chakula pia zinaweza kushiriki kwa ufanisi katika masoko ya Afrika.
Bara la Afrika ni soko kubwa na linalokua lenye zaidi ya watu bilioni 1.4 na nchi 55. Mauzo ya nje na uagizaji wa bara hili ni wa takriban dola bilioni 1500, jambo ambalo linatoa fursa za kipekee kwa Iran. Kufanyika hafla kama vile "Iranexpo 2025" na "Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Iran na Afrika" kumeandaa jukwaa linalofaa la kutambulisha uwezo wa Iran na kuvutia washirika wa Kiafrika.
Tofauti na baadhi ya nchi zinazoitazama Afrika kwa mtazamo wa kikoloni, Iran inasisitiza juu ya ushirikiano na maslahi ya pamoja, mbinu ambayo imekaribishwa na nchi za Kiafrika. Iran inajaribu kupanua uhusiano wake na nchi za Kiafrika katika fremu ya sera amilifu na iliyoratibiwa ya mambo ya nje kupitia diplomasia. Iran na nchi za Kiafrika zina mitazamo ya pamoja katika masuala mengi ya kimataifa na kutumiwa vizuri masuala hayo bila shaka kunaweza kuimarisha ushirikiano wa kisiasa wa pande mbili.
Uwepo hai wa Iran barani Afrika unaweza kusaidia kuongeza ushawishi wake kikanda na kimataifa. Kupunguza utegemezi wa masoko ya jadi na kupanua uhusiano na nchi zinazoendelea ni sehemu ya mkakati wa kiuchumi wa Iran. Usawa wa kiutamaduni na kihistoria kati ya Iran na nchi nyingi za Kiafrika pia ni msingi wa ushirikiano thabiti na wa kina.
Iran ina uzoefu mkubwa katika kubuni na kutekeleza miradi ya miundombinu, ikiwa ni pamoja na nyanja za ujenzi wa mabwawa, barabara, mitambo ya kusafisha nafuta na ya kuzalisha umeme. Nchi za Kiafrika zinakabiliwa na ukosefu wa miundombinu ya kiufundi na Iran inaweza kuwa na nafasi muhimu katika uwanja huu kwa kutuma wataalamu na makampuni yake ya uhandisi.
Mtazamo wa kibinadamu wa Iran, usio wa kudhibiti na kutawala, na unaozingatia maslahi ya pamoja utaweka msingi wa uhusiano thabiti na wenye faida kwa nchi za Kiafrika. Kwa kutumia fursa ya diplomasia hai ya kiuchumi, maonyesho maalumu na uhamishaji wa teknolojia, Iran inaweza kuwa na nafasi muhimu katika maendeleo endelevu ya Afrika na wakati huo huo kuboresha hali yake ya kiuchumi katika uga wa kimataifa.