Kauli ya Trump inathibitisha Marekani ilishirikiana na Israel moja kwa moja kuishambulia Iran
Iran imesema kuwa Marekani ilihusika moja kwa moja katika uvamizi wa utawala wa Israel dhidi yake mnamo mwezi Juni, ikinukuu kauli za hivi karibuni za Rais Donald Trump wa Marekani, kama ushahidi wa wazi wa ushiriki wa Washington katika kitendo hicho cha uchokozi.
Kupitia chapisho kwenye akaunti yake ya X siku ya Ijumaa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema kuwa kukiri kwa Trump hadharani kwamba “alisimamia kikamilifu” mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran kunathibitisha bila shaka kuwa Washington “ilishiriki kikamilifu” katika kitendo hicho “kisicho halali” cha uchokozi.
Baghaei amesema: “Kauli hii ni ushahidi usiopingika wa ushiriki wa moja kwa moja wa Marekani na ushirikiano wake wa wazi katika uvamizi wa Israeli dhidi ya Iran bila sababu ya msingi.”
Aidha, amekumbusha kuwa mwanzoni mwa vita, maafisa wa Marekani walikana kuhusika kwao katika mashambulizi hayo. Amesema: “Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, alitangaza tarehe 13 Juni 2025 kuwa Washington haikuhusika katika vita.” Rubio alinukuliwa akisema kuwa mashambulizi hayo yalikuwa “hatua ya upande mmoja” ya Israel na kwamba Marekani “haikuhusika katika mashambulizi dhidi ya Iran.”
Baghaei ameongeza: “Kauli hiyo ilikuwa uongo wa wazi, bila shaka; tangu mwanzo, ilikuwa dhahiri kuwa Marekani ilikuwa mshiriki kamili katika jinai ya uchokozi wa Israeli dhidi ya taifa la Iran.”
Mnamo tarehe 13 Juni, Israel ilianzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran, ikiwalenga na kuwaua makamanda waandamizi wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia na raia wa kawaida.
Zaidi ya wiki moja baadaye, Marekani iliingia vitani moja kwa moja kwa kushambulia vituo vitatu vya nyuklia vya Iran, kitendo kilichoashiria ukiukaji hati ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na Mkataba wa Kuzuia Ueneaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).
Mnamo tarehe 24 Juni, Iran, kupitia mashambulizi yake ya kulipiza kisasi yaliyofanikiwa dhidi ya utawala wa Israel na Marekani, iliweza kuwalazimisha maadui kusitisha uvamizi huo haramu.
Trump, akizungumza Ikulu ya White House usiku wa Alhamisi, alionekana kukiri nafasi ya Marekani katika kile ambacho awali kilielezwa na Washington kuwa ni hatua ya Israel pekee.
Alisema: “Israel ilishambulia kwanza. Shambulio hilo lilikuwa la nguvu kubwa. Nilisimamia hilo kikamilifu.”