Ni nini takwa la Tehran baada ya Trump kukiri kuhusika Marekani katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i132950-ni_nini_takwa_la_tehran_baada_ya_trump_kukiri_kuhusika_marekani_katika_mashambulizi_ya_utawala_wa_kizayuni_dhidi_ya_iran
Rais wa Marekani, Donald Trump, amekiri kuwa alikuwa na mchango katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran.
(last modified 2025-11-08T11:41:33+00:00 )
Nov 08, 2025 11:41 UTC
  • Amir Saeed Iravani
    Amir Saeed Iravani

Rais wa Marekani, Donald Trump, amekiri kuwa alikuwa na mchango katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran.

Amir Saeed Iravani, balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa alisema katika barua aliyomwandikia  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo, baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kukiri kuhusika katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran kwamba: Kwa kuzingatia kwamba kukiri kiongozi wa ngazi ya juu wa Marekani ni ushahidi wa wazi, wenye athari za kisheria kimataifa na usiopingika katika kuthibitisha namna Marekani ilivyohusika katika vitendo hivyo vya kivamizi, Marekani na utawala wa Kizayuni zinabeba dhima kikamilifu na kwa pamoja kwa hujuma hizo na matokeo yake, ikiwa ni pamoja na mauaji ya watu wasio na hatia, uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu ya raia, na kushambuliwa kwa makusudi vituo vya nyuklia vya Iran vinavyoendesha shughuli  zao kwa malengo ya kiraia. 

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kusema: Hatua hii  pia inasisitiza  haki ya msingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kufuata njia zote za kisheria za kimataifa ili kuhakikisha Marekani na maafisa wake wanawajibishwa kikamilifu na kusisistiza kulipwa fidia kamili kutokana na uharibifu uliotokea ikiwa ni pamoja na kulipwa fidia watu wote waliopoteza maisha, waliojeruhiwa na uharibifu na hasara zote zilizosababishwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na watu wake kwa mujibu wa kanuni za sheria za kimataifa. 

Rais Donald Trump wa Marekani Alkhamisi iliyopita alikiri kuwa alihusika moja kwa  moja katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran. Trump alisema alikuwa katika "udhibiti kamili" na kuongeza: "Israel ilishambulia kwanza. Lilikuwa shambulio lenye nguvu sana. Mimi nilihusika na shambuliziii hilo."

Trump amekiri kuingilia moja kwa moja katika mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya ardhi ya Iran licha ya kwamba awali alikadhibisha kuhusika katika mashambulizi hayo. Iran pia ilishasema mara kadhaa kwamba mashambulizi ya Israel dhidi yake yalifanywa kwa uratibu kamili na viongozi wa Marekani. 

Esmail Baqaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametuma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X akijiibu matamshi ya Trump na kusema kwamba: "Kukiri huku kwa Trump ni ushahidi wa wazi wa jinsi Marekani na washirika wake walivyoshiriki katika mashambulizi yasiyo na sbabu ya Israel dhidi ya Iran na wakati huo huo kukiri huko ni sawa na kukubali wazi Marekani kuwa ilichukua hatua kinyume cha sheria na kukiuka wazi sheria za kimataifa." Baqaei ametaka Marekani iwajibishwe na ibebe dhima ya hatua yake hiyo. 

Esmail Baqaei 

Kukiri Trump kwamba Marekani ilishiriki katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Tehran kunaimarisha uhalali wa kisheria wa matakwa ya Iran na kufungua njia ya kufuatiliwa kadhia  hii kimataifa. Kwa mtazamo wa kimataifa, kukiri huku kunahesabiwa kuwa ushahidi wenye mashiko na usiopingika wenye kuthibitisha kuhusika moja kwa moja Marekani katika kuvamiwa ardhi ya Iran. Kwa mtazamo wa kisheria, kitendo hiki cha Marekani ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, hasa Ibara ya 2 (aya ya 4), ambayo inakataza tishio lolote au matumizi ya nguvu na inazitaka nchi zote wanachama kuheshimu mamlaka ya kujitawala nchi, umoja wa ardhi na uhuru wa kisiasa wa mataifa mengine. Pia mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran vinavyoendesha shughuli zake kwa malengo ya kiraia na kusimamiwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ni ukiukaji wa sheria za kimataifa chini ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji na Usambazaji wa Silaha za  Nyuklia, (NPT).

Kuhusiana na kadhia hii, Iran imesisitiza katika barua yake kwamba, kukiri huko si tu kwamba kunathibitisha ubatili wa matamshi ya awali ya viongozi wa Marekani, bali pia kunatayarisha msingi wa kisheria wa kufuatilia wajibu wa Marekani na Israel kimataifa. Kwa mujibu wa sheria za uwajibikaji wa serikali katika sheria za kimataifa, serikali yoyote ambayo inashiriki katika vitendo visivyo halali inalazimika kufidia uharibifu iliousababisha. Iran imetaka kuwajibishwa kikamilifu Marekani na Israel kwa kuuwa raia, kuharibi miundo mbinu na kutishia usalama wa kikanda. 

Iran pia imesisitiza "haki ya asili ya kujilinda" chini ya Kifungu cha 51 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kutangaza kuwa ina haki ya kulipiza kisasi ikiwa uchokozi dhidi yake utaendelea.

Kwa ujumla, kukiri  kwa Trump ni nukta muhimu ya kisheria kwa Iran ambayo inaweza kufungua njia ya kuchukua hatua za kidiplomasia, kisheria na hata za kimahakama katika taasisi za kimataifa. Fursa hii ni mtihani kwa Baraza la Usalama kuonyesha kwamba halitakaa kimya mbele ya ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa.