Tehran yapuuzilia mbali madai ya Israel ya njama ya kumuua balozi wa utawala huo huko Mexico
-
Esmaeil Baqaei
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amepuuza vikali madai ya Israel kwamba Tehran ilijaribu kumuua balozi wa utawala huo nchini Mexico, akiyata madai hayo kuwa "hayana msingi na ni ya kipuuzi kabisa."
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kila wiki leo Jumatatu, Esmaeil Baqaei amesema madai hayo ni sehemu ya "mipango ya utawala wa Kizayuni ya kuharibu uhusiano wa kirafiki wa Iran na nchi zingine."
"Jambo la kupewa mazingatio ni kwamba kwa nini wamechagua Mexico? Mojawapo ya sababu za jambo hili ni kulipiza kisasi kwa maoni ya umma wa Mexico, ambao umeelezea maoni yake waziwazi katika miezi ya hivi karibuni katika kupinga mauaji ya kimbari huko Gaza," amesema Esmaeil Baqaei.
Ameongeza kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Mexico na huduma za ujasusi zimekanusha madai ya kuwepo njama kama hiyo, na kusisitiza kwamba shutuma za uongo kama hizo zilitolewa hapo awali na Australia, na baadaye ilibainika kuwa hazikuwa na msingi.
Akizungumzia kukiri kwa Rais wa Marekani Donald Trump hadharani kwamba Marekani ilihusika pakubwa katika mashambulizi wa Israel dhidi ya Iran mwezi Juni, Baqaei amesema kwamba Tehran "imesajili kukiri kwa Trump kama hati katika Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama."
Majuzi, ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Mexico ulichapisha ujumbe kwenye jukwaa la X , ukiyataja madai ya kuwepo mpango wa kumuua balozi wa Israel nchini humo kuwa ni uzushi wa kipropaganda unaolenga kuharibu uhusiano wa kirafiki na wa kihistoria kati ya Tehran na Mexico.
"Tuhuma kuhusu eti jaribio la Iran la kumuua balozi wa utawala wa Israel huko Mexico ni uzushi wa kivyombo vya habari na uongo mkubwa, ambao lengo lake ni kuharibu uhusiano wa kirafiki na wa kihistoria kati ya nchi zote mbili (Mexico na Iran); tunaupinga kabisa," umesema ujumbe wa ubalozi wa Iran huko Mexico kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Wakati huo huo, serikali ya Mexico imetangaza kwamba "haina taarifa yoyote kuhusu shambulio linalodaiwa kumlenga balozi wa Israel nchini Mexico."
Taarifa ya pamoja kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Usalama wa Ndani ya Mexico imesema hakuna ripoti za madai ya shambulio dhidi ya balozi wa Israel nchini, na kwamba Mexico haikupokea taarifa zozote zinazothibitisha madai ya njama dhidi ya balozi huyo.