Araqchi: Magharibi haina chaguo ila kuitambua Iran kama 'kitovu cha sayansi ya nyuklia'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i133048-araqchi_magharibi_haina_chaguo_ila_kuitambua_iran_kama_'kitovu_cha_sayansi_ya_nyuklia'
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema kuwa nchi za Magharibi hatimaye hazitakuwa na budi ila kuitambua Iran kama kitovu cha kisayansi cha sekta ya amani ya nyuklia.
(last modified 2025-11-11T07:58:17+00:00 )
Nov 11, 2025 07:58 UTC
  • Araqchi akikagua miradi ya nyuklia ya Iran
    Araqchi akikagua miradi ya nyuklia ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema kuwa nchi za Magharibi hatimaye hazitakuwa na budi ila kuitambua Iran kama kitovu cha kisayansi cha sekta ya amani ya nyuklia.

Sayyid Abbas Araqchi jana Jumatatu alitembelea Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) na kuangazia juhudi kubwa za Iran za kuendeleza sekta yake ya nyuklia. Amesisitiza kuwa Iran kamwe haitaacha haki zake katika sekta hii.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amepongeza maendeleo makubwa ya nchi hii katika teknolojia ya nyuklia, ambayo imestawi na kuwa sekta kubwa inayopiga hatua kwa kasi katika nyanja mbalimbali.

Amesema uwezo wa nyuklia wa Iran ni zaidi ya kurutubisha urani na unajumuisha matumizi mbalimbali katika uga wa dawa, afya, ulinzi wa mazingira, kilimo na viwanda. 

Abbas Araqchi ameeleza kuwa, wasiwasi mkubwa wa nchi za Magharibi si juu ya uwezekeno wa Iran kuunda silaha za nyuklia, bali wasiwasi wao unatokana na maendeleo ya nchi hii katika sayansi ya nyuklia.

"Iran imefaulu katika uga wa sayansi "tata na nyeti" ambayo nchi za Magharibi zinataka kuihodhi," amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran. 

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza kuwa hili limezifanya nchi za Magharibi kutumia silaha za nyuklia kama kisingizio cha kuhalalisha hatua zao.