Kwa nini Iran inaunga mkono mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi ya Sudan?
-
Hassan Shah Hosseini, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Sudan katika mazungumzo yake na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza uungaji mkono wa Tehran kwa haki ya mamlaka ya kujitawala Sudan.
Hassan Shah Hosseini, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Sudan ametoa sisitizo hilo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo, Muh al-Din Salem Ahmed, Jumapili ya tarehe 9 Novemba katika mji wa bandari wa Port Sudan, mashariki mwa Sudan.
Katika kikao hicho, Shah Hosseini aliwasilisha ujumbe wa maandishi kutoka kwa Seyyed Abbas Araqchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan kuhusu masuala yanayohusiana na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Amesisitiza msimamo thabiti wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuunga mkono mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi ya Sudan na ametaka kuwepo ushirikiano na uratibu wa nchi hizo mbili ili kukabiliana na njama za kigeni.
Balozi wa Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inasimama pamoja na nchi ya Sudan na kulaani jinai za kinyama na za kigaidi zinazofanywa na wanamgambo waasi katika mji wa el-Fasher uliopo katika jimbo la Darfur Kaskazini. Shah Hosseini amesema kuwa Iran imelaani vitendo hivyo vya kinyama nchini Sudan katika ngazi zote.
Katika kikao hicho Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Muh al-Dinn Salem pia ametoa shukurani zake kwa serikali na wananchi wa Iran kwa kuitetea Sudan na kusisitiza kuwa. uhusiano wa Khartoum na Tehran ni wa kidugu.
Hapo awali, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei alieleza wasiwasi wake kuhusu mapigano ya silaha katika mji wa el-Fasher, katikati mwa Darfur Kaskazini, Sudan, na kulaani uharibifu wa miundombinu na mauaji ya watu wasio na hatia katika mji huo.
Baghaei ameongeza kuwa: "Tunaamini kuwa uingiliaji wowote wa masuala ya ndani ya Sudan na nchi nyingine za eneo utasababisha uharibifu na madhara makubwa sio tu kwa nchi hizo, bali pia katika eneo zima."
Duru mpya ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ilianza Aprili 15, 2023, kati ya jeshi linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) vinavyoongozwa na Mohammed Hamdan Dagalo baada ya kutofautiana kuhusu mamlaka na mvutano kuhusu jinsi ya kujumuishwa Vikosi vya RSF katika jeshi baada ya mapinduzi ya 2021, na kufikia sasa upatanishi wa kimataifa haujawa na matunda.
Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imekuwa ikijaribu kupanua uhusiano wake na nchi za Afrika, ikiwemo Sudan. Tehran inaunga mkono mamlaka ya Sudan ili kuonyesha mshikamano na nchi huru za Afrika, kuimarisha uhusiano wa pande mbili, na kuchukua msimamo dhidi ya uingiliaji wa mataifa ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi zingine.
Kuunga mkono mamlaka ya Sudan na umoja wa ardhi ya nchi hiyo ni sehemu ya sera ya kikanda na kimataifa, ambayo inafuatilia malengo kadhaa:
Kuimarisha uhusiano wa pande mbili
Mazungumzo na vikao vya kidiplomasia kati ya viongozi wa Iran na Sudan kikiwemo kikao cha balozi wa Iran na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan vimesisitiza kustawishwa kwa ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Mahusiano haya yanaweza kusaidia kuongeza ushawishi wa Iran barani Afrika.
Kukabiliana na uingiliaji wa kigeni
Iran daima imekuwa ikipinga uingiliaji kati wa kijeshi na kisiasa wa madola ya Magharibi katika nchi huru. Kuiunga mkono Sudan dhidi ya vitisho vya nje, ikiwa ni pamoja na migogoro ya ndani na mashinikizo ya kimataifa, ni sehemu ya utendaji huu.
Kushikamana na mataifa ya Kiislamu na madhulumu
Sudan ni nchi ya Kiislamu yenye historia ya migogoro ya ndani na mashinikizo kutoka nje. Iran imejaribu kuonyesha mshikamano wake wa kibinadamu na Kiislamu kwa kulaani mashambulizi dhidi ya raia katika miji kama el-Fasher.
Kwa ujumla, uungaji mkono wa Tehran kwa mamlaka ya kujitawala Sudan sio tu kwamba ni hatua ya kidiplomasia bali pia ni sehemu ya sera kuu za Iran za kuimarisha uhuru na mamlaka ya kujitawala mataifa, kukabiliana na ushawishi wa Magharibi na kupanua uhusiano ma ulimwengu wa Kiislamu na Afrika.