Televisheni ya Kiebrania ya Iran yazua wasiwasi katika vyombo vya habari vya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i133912-televisheni_ya_kiebrania_ya_iran_yazua_wasiwasi_katika_vyombo_vya_habari_vya_israel
Press TV ya Iran imezindua kitengo cha lugha ya Kiebrania jambo ambalo limezua hofu katika duru za vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel kwani hatua hiyo inaonekana kama sehemu ya juhudi za kimkakati za Iran kuathiri maoni ya Waisraeli huku kukiwa na vita vya simulizi vinavyozidi kupamba moto.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Dec 04, 2025 08:33 UTC
  • Televisheni ya Kiebrania ya Iran yazua wasiwasi katika vyombo vya habari vya Israel

Press TV ya Iran imezindua kitengo cha lugha ya Kiebrania jambo ambalo limezua hofu katika duru za vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel kwani hatua hiyo inaonekana kama sehemu ya juhudi za kimkakati za Iran kuathiri maoni ya Waisraeli huku kukiwa na vita vya simulizi vinavyozidi kupamba moto.

Tangu kuzinduliwa kwake rasmi mwishoni mwa mwezi uliopita, huduma ya lugha ya Kiebrania ya Press TV imeibua gumzo katika  vyombo vya habari vya Kizayuni, huku wachambuzi wengi wakitoa maoni yanayoonyesha hofu na wasiwasi. Huduma hiyo, inayotolewa na Press TV ambayo ni sehemu ya Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB World Service), ilianzishwa ili kuwafikia wanaozungumza Kiebrania kote duniani.

Huduma hiyo inapatikana kupitia akaunti ya X (@PresstvHebrew) na kituo maalumu cha Telegram (@PresstvHebrew), huku tovuti kamili ikitarajiwa kuzinduliwa katika miezi ijayo.

Kwa mujibu wa Dkt. Ahmad Noroozi, Mkurugenzi wa IRIB World Service, jukumu kuu la kituo hicho ni kufichua ukweli ambao vyombo vya habari vya Kizayuni vinajaribu kuuficha, hasa kutokana na udhibiti mkali uliowekwa kwa vyombo vya habari vya Kiebrania katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu wakati wa vita vya siku 12.

Uzinduzi wa huduma ya Kiebrania ulifuatia azimio la Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni la Iran, lililoelekeza IRIB kuanzisha televisheni ya kimataifa ya lugha ya Kiebrania. Baraza hilo, likiongozwa na Rais Masoud Pezeshkian, limesema mpango huo unalenga kukabiliana na propaganda za utawala wa Kizayuni na vyombo vyake, kuimarisha diplomasia ya vyombo vya habari vya Iran, na kutoa taswira sahihi zaidi ya matukio ya kieneo.

Tangu kuzinduliwa kwake, vyombo vya habari vya Kizayuni vimekuwa na taharuki, vikilieleza kuwa hiyo ni  sehemu ya “vita vya simulizi” na jaribio la moja kwa moja la vyombo vya habari vya Iran kushawishi jamii ya walowezi wa Kizayuni.

Kwa mfano, tovuti ya habari ya Kizayuni Walla ilichapisha ripoti yenye kichwa: “Iran Yazindua Kituo cha Televisheni cha Kiebrania, Ikimpiku Netanyahu na Kuzungumza Moja kwa Moja na Waisraeli.” Ripoti hiyo ilikieleza kituo cha Kiebrania kama sehemu ya “juhudi za propaganda za Tehran” zilizoanzishwa kuingiza simulizi za Iran moja kwa moja katika anga ya vyombo vya habari vya Kiebrania bila wapatanishi.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa vyombo vya habari, ripoti hizi zinadhihirisha hofu na wasiwasi katika duru za kisiasa na za habari za utawala wa Kizayuni wa Israel, ambazo kwa muda mrefu zimefuata sera ya kuficha habari na uchambuzi unaoonyesha udhaifu wa utawala huo, hata katikati ya vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza.