Iran, Russia zasisitiza kutekeleza mkataba wa ushirikiano wa kimkakati katika mazungumzo ya Pezeshkian na Putin
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i134240-iran_russia_zasisitiza_kutekeleza_mkataba_wa_ushirikiano_wa_kimkakati_katika_mazungumzo_ya_pezeshkian_na_putin
Rais Masoud Pezeshkian jana Ijumaa alikutana na kuzungumza na Rais Vladimir Putin wa Russia pambizoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Amani na Uaminifu uliofanyika huko Ashgabat mji mkuu wa Turkmenistan na kusisitiza kuhusu azma thabiti ya Iran ya kutekeleza makubaliano kuhusu ushirikiano wa kina wa kimkakati kati yake na Russia.
(last modified 2025-12-12T23:04:51+00:00 )
Dec 12, 2025 23:04 UTC
  • Iran, Russia zasisitiza kutekeleza mkataba wa ushirikiano wa kimkakati katika mazungumzo ya Pezeshkian na Putin

Rais Masoud Pezeshkian jana Ijumaa alikutana na kuzungumza na Rais Vladimir Putin wa Russia pambizoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Amani na Uaminifu uliofanyika huko Ashgabat mji mkuu wa Turkmenistan na kusisitiza kuhusu azma thabiti ya Iran ya kutekeleza makubaliano kuhusu ushirikiano wa kina wa kimkakati kati yake na Russia.

Rais wa Iran amesema ameridhishwa na uhusiano unaokua kati ya Tehran na Moscow na na kupongeza uungaji mkono waRussia kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika makongamano ya kimataifa. 

Akizungumzia mkataba wa muda mrefu wa ushirikiano wa kimkakati uliotiwa saini na Iran na Russia mwezi Januari mwaka huu, Rais wa Iran amesema:"Tumedhamiria kutekeleza makubaliano hayo."

Pezeshkian pia amegusia ushirikiano wa kilimo kati ya nchi mbili kuwa ni wa manufaa makubwa, na kusema  kuwa ushirikiano huu unaweza kupanuliwai pia katika nyanja nyingine. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa ili kukabiliana na hatua na misimamo ya upande mmoja, hakuna mbadala ila ushirikiano wa pamoja, hasa kupitia mashirika ya kimataifa na kikanda kama vile Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na BRICS. 

Katika mazungumzo hayo, Rais Putin wa Russia amesema: Uhusiano wa nchi yake na Iran unastawi vyema. 

Aidha amebainisha kuwa nchi hizo mbili zinajadili kushirikiana katika sekta za gesi na nishati ya umeme, na kufanya kazi kwa karibu kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran.

"Moscow na Tehran zinashirikiana katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kinu cha nyuklia cha Bushehr na miradi ya maendeleo ya miundombinu, kama vile ukanda wa Kaskazini-Kusini," aliongeza Rais wa Russia. 

Rais Putin amesema, biashara kati ya Russia na Iran iliongezeka kwa asilimia 13 mwaka jana, na kwa asilimia nyingine 8 mwaka huu. Iran na Russia zote zinakabiliwa na vikwazo haramu vya Magharibi. Nchi mbili hizi zimeimarisha uhusiano kati yao katika nyanja mbalimbali.