Mkutano wa Tehran; Ubunifu wa Iran kwa ajili ya mwafaka wa kikanda na uthabiti wa Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i134344-mkutano_wa_tehran_ubunifu_wa_iran_kwa_ajili_ya_mwafaka_wa_kikanda_na_uthabiti_wa_afghanistan
Mkutano wa wawakilishi maalum wa nchi jirani za Afghanistan pamoja na Russia umefanyika katika wizara ya mambo ya nje ya Iran, mjini Tehran.
(last modified 2025-12-15T14:59:05+00:00 )
Dec 15, 2025 14:59 UTC
  • Mkutano wa Tehran
    Mkutano wa Tehran

Mkutano wa wawakilishi maalum wa nchi jirani za Afghanistan pamoja na Russia umefanyika katika wizara ya mambo ya nje ya Iran, mjini Tehran.

Mkutano huu, uliofanyika Jumapili tarehe 14 Disemba kwa uratibu wa Iran, ulikuwa na lengo la mashauriano na kubadilishana mawazo kuhusu matukio yanayoendelea kujiri Afghanistan, na kutafuta suluhisho ili kuimarisha uthabiti na usalama katika eneo lote.

Seyyid Abbas Araghchi, waziri wa mambo ya nje wa Iran, alisema katika mkutano huo kwamba: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kama jirani  wa Afghanistan na mshirika wa karibu wa wananchi wa nchi hiyo, daima imesisitiza juu ya kujumuishwa kwa kina kwa Afghanistan katika ukanda huu.”

Araghchi aliongeza: “Tumejifunga na kanuni hii kwamba mabadiliko na masuala ya kikanda yanaweza kusimamiwa tu kupitia mazungumzo ya kujenga, ushiriki hai wa mataifa yote, kuheshimiana kwa dhati, na kutumia mbinu za kiasili pamoja na ushirikiano wa kudumu kati ya nchi za eneo hili.”

Waziri wa mambo ya nje wa Iran pia alisema:“Mkutano huu unajumuisha wawakilishi maalum wa nchi jirani za Afghanistan pamoja na Russia, na kwa hakika ni mkutano wa kikanda wenye lengo la kuchunguza hali ya sasa katika ukanda, hususan mabadiliko yanayohusiana na Afghanistan.”

Araghchi alisisitiza: “Amani na uthabiti wa eneo tunauona tu ndani ya mfumo wa kikanda, bila kuingiliwa na mataifa ya nje au vikosi vya kigeni. Afghanistan kwa muda mrefu imekuwa ikiteseka kutokana na uwepo wa vikosi vya kigeni, uvamizi, na hasa miongo miwili ya uwepo wa Muungano wa Kijeshi wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO) pamoja na vikosi vya Marekani. Uwepo huu umeleta masaibu makubwa kwa wananchi wa Afghanistan.”

Katika mkutano huu, kwa mara ya kwanza, wawakilishi maalum wa nchi jirani za Afghanistan (Pakistan, China, Tajikistan, Turkmenistan, Uzbekistan) pamoja na Russia walikusanyika mjini Tehran.

Lengo kuu lilikuwa ni kuimarisha uratibu na mshikamano wa kikanda kwa ajili ya kusimamia na kukabili mgogoro wa Afghanistan.

Iran na nchi zilizoshiriki katika mkutano wa Tehran zilisema kwa msisitizo kwamba hakuna suluhisho lililoandaliwa nje ya ukanda linaloweza kutatua matatizo ya Afghanistan. Washiriki wamesema kuwa ni majirani pekee wa Afghanistan, kwa kuzingatia uhusiano wa kihistoria, kitamaduni na kiusalama, ndio wanaoweza kutoa njia za kudumu na thabiti za kutatua changamoto hizo.

Mkutano huu ulifanyika katika hali ambayo uhusiano kati ya Afghanistan na Pakistan umekumbwa na mvutano mkali, huku mazingira ya kiusalama yakiwa dhaifu na hatarishi.

Kwa hivyo, mazungumzo ya Tehran yalionekana kama fursa ya kupunguza mvutano huo na kutafuta suluhisho la pamoja miongoni mwa majirani wa Afghanistan. 

Mikakati ya Iran kwa ajili ya kuleta uthabiti nchini Afghanistan na katika ukanda mzima imejengeka juu ya mazungumzo yenye manufaa, mshikamano wa kikanda, ushiriki hai wa majirani, kuheshimiana kwa dhati na kutumia mbinu za kiasili za eneo.

Iran inaamini kwamba suluhisho pekee la kudumu ni ushirikiano wa nchi za ukanda bila kuingiliwa na vikosi vya nje ya eneo.

Iran imesisitiza kwamba mgogoro wa Afghanistan unaweza kusimamiwa tu kupitia mazungumzo baina ya nchi za ukanda na ushiriki hai wa majirani wote. Mazungumzo haya yanapaswa kujengeka juu ya kuheshimiana kwa dhati na maslahi ya pamoja.

Iran daima imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kuingizwa kwa kina kwa Afghanistan katika miundo ya maamuzi na taasisi za kikanda. Ujumuishaji huu unaweza kuwa msingi wa maendeleo ya kiuchumi, usalama wa kudumu na kupunguza mvutano wa kisiasa.

Mkutano wa Tehran ulioshirikisha Iran, Russia na majirani wengine wa  Afghanistan yaani Pakistan, China, Tajikistan, Turkmenistan, Uzbekistan,  unaonyesha juhudi za Iran za kuunda mwafaka wa kikanda kuhusu mabadiliko yanayoendelea kushuhudiwa Afghanistan. Mshikamano huu unaweza kuimarisha usalama wa pamoja na kupunguza vitisho vya kawaida kama vile ugaidi na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Iran imetangaza kuwa matokeo ya mikutano ya kikanda yatawasilishwa kwa serikali ya Afghanistan, na inalenga kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na ya kudumu na watawala wa sasa wa Afghanistan ili kuweka msingi wa ushirikiano wa vitendo.

Kufanyika kwa mkutano wa wawakilishi maalum wa majirani wa Afghanistan pamoja na Russia mjini Tehran ni ishara ya ubunifu wa Iran katika diplomasia ya kikanda na jitihada za kutatua mgogoro wa Afghanistan kupitia suluhisho la kieneo na ushirikiano wa kudumu.