Kwa nini Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai inapinga uingiliaji wa kigeni nchini Iran?
Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) imetangaza rasmi kupinga uingiliaji wa aina yoyote wa kigeni nchini Iran.
Kuhusiana na hilo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai amemtumia ujumbe Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran akisisitiza upinzani wake dhidi ya uingiliaji wowote wa kigeni katika masuala ya ndani na kudhoofishwa umoja na mshikamano wa wananchi wa Iran.
Nurlan Yermekbayev, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai amesisitiza katika ujumbe wake kwa Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran kuwa, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai daima inatilia mkazo kuheshimiwa sheria na mamlaka ya kujitawala, uhuru na umoja wa ardhi ya nchi wanachama. Pia inapinga jaribio lolote la majeshi ya kigeni kuingilia masuala ya ndani ya nchi wanachama na kudhoofishwa mshikamano na umoja wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.
Katika miaka ya hivi karibuni, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai imekuwa ikitangaza waziwazi upinzani wake dhidi ya uingiliaji wowote wa kigeni nchini Iran. Msimamo huu unatokana na vipengele vya usalama, kijiografia, kisiasa na kiuchumi ambavyo vinaweza kuchanganuliwa ndani ya mfumo wa malengo makuu ya jumuiya hiyo. Jumuiya ya Shanghai, ambayo sasa inachukuliwa kuwa moja ya kambi muhimu zaidi za usalama katika eneo la Eurasia na Asia, inasisitiza sheria kama vile kuheshimiwa mamlaka ya kitaifa, kutoingilia masuala ya ndani ya nchi wanachama na kukabiliana na vitisho vya pamoja. Kwa hiyo, upinzani dhidi ya uingiliaji wa kigeni nchini Iran si suala la muda tu, bali ni sehemu ya muundo wa kifikra na kiusalama wa jumuia hii.
Sababu ya kwanza ya Shanghai kupinga uingiliaji wa kigeni nchini Iran ni kufuata sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa. Pamoja na mambo mengine, katika taarifa rasmi ya jumuiya hii kuhusu mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran katika kipindi cha vita vya siku 12 vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, Jumuiya ya Shanghai iliutaja uvamizi huo kuwa ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na mamlaka ya kujitawala Iran. Wanachama wa Shanghai, hasa China na Russia, daima wanasisitiza kuzingatiwa sheria za kimataifa na kuuchukulia uingiliaji wa kigeni kama tishio kwa utulivu wa eneo.
Sababu ya pili ni wasiwasi wa usalama. Iran ni mmoja wa wahusika wakuu katika usalama wa eneo la Eurasia na Asia Magharibi. Kukosekana kwa utulivu nchini Iran kunaweza kuwa na madhara makubwa kwa usalama wa nishati, mapambano dhidi ya ugaidi na uthabiti wa mipaka ya nchi wanachama wa Shanghai. Russia, katika mazungumzo yake ya kiusalama na Iran, imechukulia uingiliaji wa mataifa ya kigeni kuwa tishio kwa usalama wa eneo na kulaani vikali suala hilo. Kwa mtazamo wa wanachama wa Shanghai, ukosefu wowote wa uthabiti nchini Iran unaweza kuibua wimbi la ukosefu wa usalama katika eneo na kuvuruga njia za kusafirisha nishati.
Sababu ya tatu ni umuhimu wa kijiografia wa Iran kwa miradi mikubwa ya kikanda. Iran ndio kiunganishi kikuu kati ya Eurasia Mashariki na Magharibi na ina nafasi muhimu katika miradi ya uchukuzi, nishati na biashara. Kukosekana utulivu nchini Iran kunaweza kuvuruga miradi kama vile ya Ukanda wa Kaskazini-Kusini, Ubunifu wa Njia na Barabara Kuu pamoja na ushirikiano wa nishati. Kwa hivyo, wanachama wa Shanghai wanauchukulia utulivu wa Iran kama sehemu ya utulivu wao wa kimkakati.
Sababu ya nne ni kukabiliana na misimamo ya upande mmoja na uingiliaji wa nchi za Magharibi. Wanachama wengi wa Shanghai, haswa China na Russia, wanauchukulia uingiliaji wa kijeshi na kisiasa wa Magharibi katika nchi huru kama tishio kubwa kwa mfumo wa kambi nyingi. Kupinga uingililiaji wa kigeni nchini Iran kwa hakika ni sehemu ya juhudi za jumuiya hii kwa ajili ya kuimarisha mfumo huo na kupunguza taathira hasi za upande mmoja.
Sababu ya tano ni msimamo wa Iran kama mwanachama kamili wa Jumuiya hiyo. Tangu 2023, Iran imekuwa mwanachama rasmi wa Jumuiya ya Shanghai na uanachama huu umeongeza jukumu la jumuiya hii katika kuunga mkono usalama na uhuru wa Iran. Kusaidia mwanachama ni sehemu ya utambulisho na usalama wa pamoja wa jumuiya. Kwa kuwa Iran ina uanachama kamili katika Jumuiya ya Shanghai, uungaji mkono huu wa jumuiya umeimarishwa kama kambi ya kieneo na una maana ya kupinga mashinikizo yoyote ya nje kwa shabaha ya kubadilisha siasa za ndani za Iran.
Kwa ujumla, upinzani wa SCO dhidi ya uingiliaji wa kigeni nchini Iran unatokana na mchanganyiko wa misingi ya sheria, masuala ya usalama, maslahi ya kijiopolitiki na jitihada za kuimarisha mfumo wa pande kadhaa. Msimamo huu unaonyesha kuwa Iran ina nafasi ya kistratijia katika milingano ya kiusalama na kisiasa ya Eurasia na uthabiti wake una umuhimu mkubwa kwa wanachama wa Shanghai.