Muendelezo wa ushirikiano wa Tehran-Caracas; nembo ya muqawama dhidi ya mashinikizo ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135698-muendelezo_wa_ushirikiano_wa_tehran_caracas_nembo_ya_muqawama_dhidi_ya_mashinikizo_ya_marekani
Rais wa muda wa Venezuela amesisitiza kwamba, Caracas itaendeleza uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-01-20T08:52:20+00:00 )
Jan 20, 2026 08:52 UTC
  • Rais wa uongozi wa muda wa Venezuela, Delcy Rodriguez,
    Rais wa uongozi wa muda wa Venezuela, Delcy Rodriguez,

Rais wa muda wa Venezuela amesisitiza kwamba, Caracas itaendeleza uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais wa uongozi wa muda wa Venezuela, Delcy Rodriguez, amebainisha kwamba Caracas ina haki ya kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na China, Cuba, Iran na Russia na kupinga vikali uingiliaji wa Marekani. Aidha amekosoa hatua za kichokozi za Washington dhidi ya nchi hiyo.

Matamshi ya Rais wa muda wa Venezuela yanatolewa wakati ambapo Ismail Baghaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hapo awali alikuwa amesisitiza kuendelezwa uhusiano wa Caracas na Tehran, akisema: "Uhusiano wetu na Venezuela umekuwa ukitegemea msingi wa heshima na maslahi ya pande zote, na tunatumai kwamba uhusiano huu utaendelea."

Baada ya wiki chache za shambulio la kijeshi la Marekani dhidi ya Venezuela na kutekwa nyara Rais Nicolas Maduro, misimamo ya viongozi ya Caracas imeingia katika awamu iliyo wazi na yenye maana zaidi; kiasi kwamba, msisitizo wa Rodriguez, rais wa muda wa Venezuela, kuhusu mwendelezo wa uhusiano wa nchi yake na Iran unapaswa pia kutathminiwa katika fremu hii; hasa kwa kuwa maneno haya yametolewa katika hali ambayo hali ya kisiasa nchini Venezuela bado iko chini ya ushawishi wa uingiliaji kati wa moja kwa moja wa kijeshi wa Washington na njama za Marekani za kulazimisha matakwa yake kwenye muundo wa madaraka huko Caracas.

Matamshi haya yanapata umuhimu maradufu tunapochunguza muktadha wa upinzani dhahiri dhidi ya madai ya Donald Trump na sera ya Marekani ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa. Serikali ya Marekani, ambayo katika miaka iliyopita iliweka vikwazo, ilitoa vitisho na kuingilia mambo ya ndani ya Venezuela na kuligeuza hilo kuwa, wenzo mkuu wa diplomasia yake dhidi ya nchi hiyo, sasa inajaribu kufafanua upya njia ya kisiasa ya baadaye ya Caracas kwa kuchukua hatua za moja kwa moja za kijeshi kwa kumteka nyara rais halali wa nchi hiyo. Hata hivyo, msisitizo wa rais wa muda wa Venezuela wa kuendeleza uhusiano wake na Iran unatuma ujumbe wa wazi na dhahiri shahiri kwa Washington kwamba: Mashinikizo, vitisho na hata hatua za kijeshi haziwezi kuilazimisha Venezuela na kuifanya ilegeze kamba au irejee na kuachana na misimamo yake thabiti.

Nicolas Maduro 

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, kuendelea kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wakati huu kabla ya kuwa ni zaidi ya chaguo la kidiplomasia tu, hatua hiyo imekuwa ishara ya kutotii mfumo uliotwishwa na Marekani. Kwa msimamo huu, Caracas inaonyesha kwamba, haiko tayari kutoa kafara uhuru na mamlaka yake ya kitaifa na inaiona kuwa ni haki yake ya wazi ya kufanya maamuzi kuhusu mahusiano ya kigeni. Mbinu hii, hasa baada ya kutekwa nyara Nicolás Maduro, imepata maana zaidi ya wakati uliopita na imekuwa sehemu ya mazungumzo ya muqawama wa kisiasa dhidi ya uchukuaji maamuzi ya upande mmoja wa Marekani.

Katika wigo mpana zaidi, uhusiano wa Venezuela na Iran una vipengele muhimu vya kisiasa. Nchi zote mbili zimekabiliwa na vikwazo vikubwa, mashinikizo ya kidiplomasia, na njama za kubadilisha muundo wa madaraka kutoka nje kwa miaka mingi. Tajiriba na uzoefu huu wa pamoja umefungua njia ya kuwemo mitazamo mimoja ya kisiasa kati ya Tehran na Caracas; misimamo mimoja ambayo inajaribu kuwasilisha simulizi mpya ya utaratibu wa kimataifa; ambapo nchi hazilazimiki kuifurahisha Washington ili kujipatia uhalali au kubakai hai, bali zinaweza kuunda miungano yao huru kulingana na maslahi ya pande mbili. Kwa mtazamo huu, msisitizo wa kuendelezwa uhusiano na Iran ni aina ya ufafanuzi mpya wa uhuru na mamlaka ya kitaifa, ambayo yanapinga uingiliaji kati wa kigeni na kuegemeza sera yake ya kigeni kwenye uhuru, mamlaka ya kujitawa na ushirikiano wa pande nyingi.

Katika upande wa kiuchumi, uhusiano wa Tehran-Caracas ni jibu la kivitendo kwa hali halisi ya kiuchumi. Nchi zote mbili zinakabiliwa na vikwazo vikubwa katika kufikia masoko ya fedha duniani na teknolojia za hali ya juu. Kwa hivyo, ushirikiano katika maeneo kama vile nishati, usafirishaji, kilimo na ubadilishanaji wa bidhaa utaipa fursa Venezuela ya kupunguza baadhi ya mashinikizo ya kiuchumi na kutafuta njia mbadala za kukidhi mahitaji yake ya lazima.

Mbali na uchumi na siasa za pande mbili, msisitizo wa kuendeleza uhusiano na Iran una ujumbe mpana kwa jamii ya kimataifa. Kwa kuchagua njia huru, Venezuela inatangaza kwamba, sera ya kigeni haiwezi kuamuliwa na vitisho, vikwazo, au hatua za kijeshi. Msimamo huu unaambatana na kanuni za kimsingi za sheria ya kimataifa na kanuni ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine; kanuni ambazo serikali ya Marekani imezipuuza mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni, hasa kuhusu Venezuela. Kwa kutetea haki yake ya kuchagua washirika wa kimataifa, Venezuela inajaribu kuonyesha kwamba bado inawezekana kupinga hatua za upande mmoja za Marekani.

Hatimaye, msisitizo wa rais wa muda wa Venezuela kuhusu kuendeleza nchi yake uhusiano na Iran unapaswa kuzingatiwa kama uamuzi halali, wenye weledi na uliojengeka juu ya msingi wa maslahi ya kitaifa; uamuzi ambao si jibu la muda tu kwa mashinikizo ya Marekani, bali ni sehemu ya mkakati mkuu wa Caracas wa kudumisha uhuru wa kisiasa, kujenga upya uwezo wa kiuchumi, na kufafanua upya nafasi yake katika nidhamu na utaratibu wa kimataifa.