Araqchi: Tatizo la sasa la Ulaya ni matokeo ya usaliti wake wa huko nyuma dhidi ya Iran
-
Sayyid Abbas Araqchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema Ulaya sasa inasumbuliwa na matokeo ya usaliti wake wa zamani kwa Iran na inakabiliwa na unyanyasaji kama huo kutoka kwa Marekani.
Sayyid Abbas Araqchi ametoa matamshi hayo katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X mapema leo Jumatano, akikumbusha jinsi mataifa ya Ulaya yalivyokiuka makubaliano ya nyuklia na Jamhuri ya Kiislamu, ambayo yalisainiwa mwaka 2015, kwa mujibu wa takwa la Washington. Usaliti huo ulishuhudia mataifa matatu ya Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani yakisitisha biashara zao na Iran baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia mwaka wa 2018.
Sayyid Araqchi anasema, nchi hizo hizo za Ulaya, ambazo zilitii Marekani kwa kutoheshimu makubaliano hayo, sasa zinalazimika kustahamili "matokeo mabaya" ya usaliti huo.
Araqchi amesisitiza katika ujumbe huo kwamba: "Donald Trump alipofuta makubaliano ya nyuklia ya Iran kwa upande mmoja wakati wa muhula wake wa kwanza wa urais, Troika ya Ulaya na Umoja wa Ulaya zilimfuata kwa imani thabiti na hata kumsaidia. Kwa kufanya hivyo, walipaswa kuzingatia matokeo haya ya leo."
"Somo la wazi na dhahiri linaweza kutolewa kutokana na matukio haya: ama "mikataba yote ni mikataba," au "kupeana mikono hakuna thamani." Mfano mkuu wa suala hili ni tishio la Trump la kuivamia Greenland kwa njia yoyote inayowezekana, ambayo, japokuwa ni kinyume kabisa cha sheria za kimataifa lakini Ulaya inastahili kufanyiwa hivyo" amesisitiza Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, amemnukuu Ursula von der Leyen, Rais wa Tume ya Ulaya, akijibu tishio la Rais wa Marekani kwa kudai kwamba Trump analazimika kuheshimu makubaliano yake na Brussels na kusema: "Katika siasa, kama ilivyo katika biashara, makubaliano ni makubaliano" na pande mbili zinaposhikana mikono, lazima makubaliano yaheshimiwe."
Sayyis Abbas Araqchi amesisitia kwa kusema: Inasikitisha kwamba, kwa Umoja wa Ulaya, tatizo lake la sasa ndilo hasa linaloitwa "athari kinyume."