Kwa nini Iran inatilia mkazo kuhusu haki yake ya kurutubisha urani kwa ajili ya malengo ya amani?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135734-kwa_nini_iran_inatilia_mkazo_kuhusu_haki_yake_ya_kurutubisha_urani_kwa_ajili_ya_malengo_ya_amani
Iran imetangaza kuwa abadan haitaacha haki yake ya kurutubisha madini ya urani kwa malengo ya kiraia.
(last modified 2026-01-21T10:02:09+00:00 )
Jan 21, 2026 10:02 UTC
  • Kwa nini Iran inatilia mkazo kuhusu haki yake ya kurutubisha urani kwa ajili ya malengo ya amani?

Iran imetangaza kuwa abadan haitaacha haki yake ya kurutubisha madini ya urani kwa malengo ya kiraia.

Ali Bahraini, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi alisema jana katika Mkutano wa Upokonyaji Silaha kwamba Tehran kamwe haitaacha haki yake ya kurutubisha urani kwa ajili ya malengo ya kiraia. 

Bahraini amelaani mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani na utawala wa Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran na kuitaja hujuma hiyo kuwa ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na pigo kubwa kwa Mkataba wa Kuzuia Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).

Bahraini ameashiria matukio ya mwaka 2025, mashambulizi ya Juni 13 yaliyoanzishwa na utawala wa Israel dhidi ya umoja wa ardhi na uhuru wa kisiasa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa mashambulizi hayo yalikuwa kinyume cha sheria, yaliyopangwa mapema na yaliyokiuka kanuni za sheria za kimataifa na kuongeza kuwa: 'Katika muendelezo wa chokochoko hizo; tarehe 22 mwezi Juni mwaka jana Marekani ilikiuka kanuni za mkataba wa NPT na kuvishambulia vituo vya nyuklia vya Iran huko Fordow, Natanz, na Isfahan vinavyoendesha shughuli zake kwa usimamizi wa IAEA; hatua ambayo ni tishio kuu kwa amani na usalama wa kimataifa na Mkataba Unaopiga Marufuku  Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT). 

Mwakilishi wa Iran amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajibu kitendo chochote cha uchokozi ndani ya fremu ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na kwamba kurutubisha madini ya urani kwa malengo ya amani ni haki ya wazi na isiyopingika ya Iran kama nchi mwanachama wa Mkataba wa NPT.  Wakati huo huo, Ali Bahraini amebainisha kuwa Iran siku zote imekuwa tayari kwa ajili ya mazungumzo ya kweli , yasiyo na masharti na kwa msingi wa kuheshimiana.

Sisitizo la Iran kuhusu haki yake ya kurutubisha urani kwa malengo ya amani unatokana na kanuni za kisheria, mahitaji ya kimkakati, uzoefu wa kihistoria na masuala ya usalama. Jambo hili si hitajio la muda bali ni sehemu ya utambulisho wa kisheria na kisiasa wa Iran kimataifa. Mkabala wake, nchi za Magharibi zinaibua madai mbalimbali kwamba upo uwezekano wa miradi ya nyuklia ya Iran kukengeuka na kujikita katika malengo ya kijeshi zikijaribu kila ziwezalo kuibana haki hii ya Iran; madai ambayo hayawezi kutetewa wala kuungwa mkono kwa mtazamo wa sheria za kimataifa na ukweli wa kiufundi.

Moja ya sababu zinazoifanya Iran itilie mkazo suala hili ni kutokana na kuwa ni haki yaie ya kisheria na isiyopingika kwa mujibu wa Mkataba wa (NPT). Mkataba huu umeeleza wazi kwamba nchi zote wanachama zina haki ya kuwa na mzunguko kamili wa mafuta ya nyuklia, ikiwa ni pamoja na urutubishaji wa madini ya urani kwa matumizi ya amani. Iran ikiwa ni mwanachama wa Mkataba wa NPT si tu ina haki hii tajwa, bali pia kwa miaka kadhaa sasa imekuwa ikitekeleza shughuli zake chini ya usimamizi mkali wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), na imetangaza mara nyingi kwamba hakuna ukengeukaji wowote ulioshuhudiwa katika miradi yake ya nyuklia. Kwa msingi huo, hatua yoyote ya kupinga Iran kurutubisha urani bila shaka itakuwa ukiukaji wa wazi wa haki ya nchi mwanachama wa NPT. 

Mkataba Unaopiga Marufuku Usambazaji wa Silaha za Nyuklia NPT 

Sababu nyingine ni mahitaji halisi ya Iran ya nishati na kuwa na vyanzo mbalimbali vya nishati. Iran kutokana na idadi kubwa ya raia wake, na matumizi makubwa ya nishati haiwezi kutegemea tu rasilimali za mafuta. Nishati ya nyuklia ni moja ya machaguo endelevu na ya kiuchumi zaidi kwa ajili ya siku zijazo. Mbali na hiili, Iran inakabiliwa na vikwazo vikubwa na haiwezi kutegemea nchi ajinabi kujidhaminia nishati ya mafuta kwa ajili ya mitambo yake ya kuzalisha umeme. Uzoefu wa nchi zinazomiliki teknolojia ya nyuklia wa kukata ushirikiano wa nyuklia na baadhi ya nchi au mashinikizo ya kisiasa ya nchi za Magharibi umeonyesha kwamba kuwa tegemezi katika sekta ya nishati kunaweza kutumika kama wenzo wa mashinikizo.  

Na mwishowe, tunaweza kusema kuwa hatua ya Iran ya kusisitiza kuhusu haki yake ya kurutubisha urani si suala la kisiasa la muda bali ni kitendo cha kutetea haki yake ya kisheria, kuwa na uhuru upande wa nishati, kupiga hatua kisayansi na kukabiliana na vigezo vya undumakuwili vya Magharibi. Tajiriba inaonyesha kuwa kurudi nyuma katika sekta  hii  kutapelekea tu kuongezeka mashinikizo na miendendo ya uhasama ya nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani. HIi ni katika hali ambayo kutilia mkazo kuhusu haki halali ya nyuklia, hasa haki ya kurutubisha madini ya urani, kutathibisha nafasi huru ya nchi hii na namna invayofungamana na sheria.