Bahreini: Iran haitafumbia macho katu haki yake ya kurutubisha urani kwa matumizi ya amani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135744-bahreini_iran_haitafumbia_macho_katu_haki_yake_ya_kurutubisha_urani_kwa_matumizi_ya_amani
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amesisitiza kwamba, taifa hili halitafumbia macho katu haki yake ya kurutubisha urani kwa ajili ya matumizi ya amani.
(last modified 2026-01-21T10:42:46+00:00 )
Jan 21, 2026 10:42 UTC
  • Bahreini: Iran haitafumbia macho katu haki yake ya kurutubisha urani kwa matumizi ya amani

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amesisitiza kwamba, taifa hili halitafumbia macho katu haki yake ya kurutubisha urani kwa ajili ya matumizi ya amani.

Ali Bahreini ametoa sisitizo hilo katika Mkutano wa Kutokomeza Silaha, ambapo sambamba na kulaani mashambulizi ya mwezi Juni 2025 yaliyofanywa na Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, amezielezea hujuma hizo kuwa ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa, na pigo kubwa kwa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT).

Huku akiipongeza Mongolia kwa kuchukua urais wa Mkutano wa Kutokomeza Silaha, Bahreini amesisitizia uungaji mkono kamili wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa juhudi za kufufua nafasi ya mazungumzo ya taasisi hii na akasema: "Mkutano wa Kutokomeza Silaha, ikiwa ni taasisi pekee ya majadiliano ya baina ya pande kadhaa katika uga wa kutokomeza silaha, inapaswa ilinde asili yake ya kusimamia majadiliano na kuzuia kuwa taasisi ya kuendesha mazungumzo matupu."

Akiashiria matukio yaliyojiri ya mwaka 2025, Bahreini amelielezea shambulio la utawala wa Israel la Juni 13 dhidi ya umoja wa ardhi yote na uhuru wa kisiasa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni la "kinyume cha sheria, lililopangwa mapema, na lililokiuka sheria za sheria za kimataifa," na akaongezea kwa kusema: "katika mwendelezo wa uchokozi huu, mnamo Juni 22, Marekani, kwa mashauriano na utawala ambao si mwanachama wa NPT, ilivilenga vituo vya nyuklia vya Iran vilivyo chini ya usimamizi huko Fordow, Natanz, na Esfahan, hatua ambayo ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa na mkataba wa NPT.

Mwakilishi wa Iran amesisitiza: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajibu mapigo kwa kitendo chochote cha uchokozi kwa kufunmgamana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa; na kurutubisha urani kwa malengo ya amani ni haki ya wazi kabisa na isiyoweza kukanushika ya Iran ikiwa ni mwanachama wa NPT, haki ambayo haitaisamehe kamwe."

Lakini sambamba na hayo, Bahreini ameeleza bayana kwamba, Iran, siku zote iko tayari kwa mazungumzo ya dhati, yasiyo na masharti, na ya msingi wa kuheshimiana kati ya pande mbili.../