Iran na Saudia katika mkondo wa ushirikiano na matarajio ya kuleta usalama, ustawi na umoja baina ya Waislamu
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed Bin Salman na kusisitiza kwamba: muelekeo inaofuata Iran katika uga wa kikanda umejengwa juu ya msingi wa udugu wa Kiislamu, kustawisha uhusiano wa kirafiki, na kupanua mashirikiano na nchi za Kiislamu.
Katika mazungumzo hayo na Bin Salman, Rais Pezeshkian amesema, muelekeo wa Iran umejengeka juu ya msingi wa kudumisha umoja na mfungamano wa jamii za makabila na dini na kuimarisha mshikamano wa kitaifa; na katika uga wa kikanda, inafanya juhudi zinazofuata muelekeo wa kuimarisha na kukuza udugu wa Kiislamu, kustawisha uhusiano wa kirafiki na kupanua mashirikiano na nchi za Kiislamu".
Rais wa Iran ameendelea kwa kusema: “kwa ushirikiano wa pamoja, tunaweza kujenga eneo salama, lililoendelea na lililopiga hatua mbele kwa ajili ya mataifa yetu.”
Pezeshkian ametoa shukurani pia kwa msukumo na uungaji mkono wa nchi za Kiislamu hususan Saudi Arabia kwa taifa la Iran na akasema: “vitisho na vita vya kisaikolojia vya Wamarekani vinalenga kuvuruga usalama wa eneo na havitakuwa na matunda yoyote kwao wao zaidi ya kuvuruga utulivu”.

Katika mazungumzo hayo ya simu na Rais Pezeshkian, Mohammed bin Salman, Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, yeye kwa upande wake alisema: “mshikamano na mfungamno wa nchi za Kiislamu una umuhimu wa hali ya juu”.
Mazungumzo ya simu ya Rais wa Iran na Mohammed bin Salman si mawasiliano ya kawaida tu ya kidiplomasia; mazungumzo hayo yanaweza kutathminiwa kama kielelezo cha muelekeo mpya, lakini uliokita mizizi kwa muda mirefu, wa sera ya nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na Ulimwengu wa Kiislamu.
Iran haijichukulii kuwa ni mdau wa kisiasa tu, bali inajihesbu pia kama mmoja wa watu wa familia kubwa ya Kiislamu ambayo ina jukumu la kimaadili na kimkakati kuhusiana na nchi zingine za Kiislamu. Kwa hivyo, ushirikiano wa pamoja nao pia ni dharura ya kimkakati. Mtazamo huu unaweka msingi wa muunganiko wa pamoja wa kiutambulisho na kimkakati katika Ulimwengu wa Kiislamu ambao unaweza kutoa mchango wa kuleta utulivu mbele ya mashinikizo na uingiliaji wa madola ya nje ya eneo.
Iran inajitambulisha kama mshirika wa sasa na baadaye wa nchi za Kiislamu katika kujenga mustakabali tofauti kwa ajili ya eneo hili, ambalo ndani yake nafasi ya mantiki ya makabiliano, inachukuliwa na mantiki ya ushirikiano na ya hatima ya pamoja. Kuchunguzwa pande mbalimbali za ushirikiano kati ya Iran na Saudi Arabia kunaonyesha kuwa, uhusiano huu unakwenda mbali zaidi ya maelewano ya kawaida ya baina ya pande mbili tu na yanaweza kubadilisha muundo wa kiusalama, kiuchumi na kisiasa wa Asia Magharibi. Uhusiano wa Tehran na Riyadh una taathira kwa Ulimwengu wa Kiislamu na hata kwa mfumo wa kimataifa.
Yakiwa ni madola mawili makuu katika Asia Magharibi, Iran na Saudi Arabia zina nafasi kuu katika kujenga michakato ya kiusalama, kisiasa na kiuchumi ya eneo hilo. Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, zaidi ya kutokana na uhusiano wa pande mbili, una matokeo yenye taathira kubwa kwa utulivu wa kikanda, kupunguza mivutano ya kimadhehebu, kudhibiti uingiliaji wa mataifa ya nje kanda hii na kwa maendeleo ya kiuchumi.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa, ustawi na maendeleo ya eneo hili vinaweza kupatikana kupitia ushirikiano wa pamoja tu. Kwa ushirikiana wa pamoja, nchi za Kiislamu zinao uwezo wa kujenga eneo lenye ustawi, usalama na uthabiti, na muelekeo huo unaiweka Iran kwenye nafasi ya kuunga mkono mashirikiano ya baina ya pande kadhaa.

Iran na Saudi Arabia ni wadau wawili muhimu katika Ulimwengu wa Kiislamu. Ushirikiano kati ya nchi hizi mbili unaweza kuwa na athari ya moja kwa moja kwa usalama, utulivu na ustawi wa eneo hili. Pande zote mbili zinatilia mkazo juu ya mshikamano wa Kiislamu na maslahi ya pamoja ya mataifa ya Waislamu. Muelekeo huu wa pamoja unaweza kuleta mabadiliko muhimu sana katika milingano ya kijiopolitiki ya Asia Magharibi.
Kwa upande wa kiuchumi pia, ushirikiano kati ya pande mbili unaweza kuwa chachu ya kuchochea ustawi na maendeleo ya kikanda. Iran na Saudi Arabia zote mbili zina fursa na uwezo mkubwa wa nishati, maliasili, masoko makubwa na kuwako kwenye nafasi muhimu sana ya kijiopolitiki. Kuunganisha pamoja fursa na uwezo wao huo kunaweza kupelekea kupatikana uthabiti katika soko la nishati, uendelezaji wa miradi ya pamoja, kuongezeka biashara na kuimarishwa njia za upitishaji bidhaa…/