Siku ya tisa ya vita; Iran yaendeleza mawimbi ya makombora na ndege zisizo na rubani
Katika siku ya tisa ya uchokozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) alfajiri ya leo limetangaza kutekelezwa kwa mawimbi mapya ya Operesheni ya kulipiza kisasi ya ‘Ahadi ya Kweli 4’
Kwa mujibu wa msemaji wa Makao Makuu ya Kamandi ya Majeshi ya Iran ya Khatam al Anbiya, katika operesheni hii ya pamoja malengo mbalimbali kuanzia kaskazini hadi kusini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) yamelengwa na kupigwa kwa usahihi kwa kutumia makombora ya aina ya Kheibar Shekan, Emad, na Qadr yenye vichwa vingi vya vilipuzi.
Wakati huohuo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilitangaza pia shambulio la kombora dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani ya Al Jufair, likielezwa kuwa ni jibu kwa shambulio lililofanywa dhidi ya kituo cha kusafisha maji cha Qeshm. Viongozi wa juu wa Jamhuri ya Kiislamu wamesisitiza kwamba mashambulizi ya kulipiza kisasi yataendelea kuwa ya kudumu na yataendelea hadi wavamizi watakapoadhibiwa kikamilifu.
Siku ya tisa ya vita vya kichokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran inaweza kuelezwa kuwa hatua ya mabadiliko makubwa katika upanuzi wa kiwango cha vita. Mazingira ya vita sasa yamegeuka na kuwa uwanja wa operesheni changamano zenye tabaka nyingi. Utekelezaji wa wimbi jipya la Operesheni Ahadi ya Kweli 4 unaonyesha kwamba Iran si tu imehifadhi uwezo wake wa kuendeleza mashambulizi kwa muda mrefu, bali pia imevuka mifumo ya rada ya adui na kufikia hatua ya kujivunia kwamba “kuziharibu shabaha za adui sasa kumezidi kuwa rahisi.”
Katika hatua muhimu zaidi, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza kuwa, kama jibu kwa uvamizi wa jeshi la kigaidi la Marekani kutoka kambi ya Jafair nchini Bahraini dhidi ya kiwanda cha kusafisha maji chumvi cha Qeshm, limeishambulia kambi hiyo kwa makombora ya kisasa yanayoongozwa kwa usahihi, yenye mafuta dhabiti.
Brigedia Naini, msemaji wa IRGC, amesema wazi kuwa: “Kambi yoyote ya kijeshi ya Marekani, popote ilipo katika eneo hili, ni shabaha halali kwa majeshi yetu.”
Aidha, kitengo cha makombora cha Jeshi la Nchi Kavu la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kililenga na kushambulia pia ngome za makundi ya kujitenga yanayoungwa mkono na Marekani katika maeneo mawili kaskazini magharibi mwa nchi. Hatua hii inaonesha kuwa Iran, sambamba na kuendesha vita katika uwanja wa nje, inaendelea kufuatilia na kulinda usalama wake wa ndani kwa msimamo thabiti na kwa uangalifu mkubwa.
Jeshi pia limetangaza leo asubuhu kuwa ndege isiyo na rubani aina ya Hermes, inayomilikiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel, ililengwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya Jeshi katika mkoa wa Markazi na ikaangushwa.
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilikuwa tayari limetangaza jana, katika taarifa yake namba 16, kwamba tangu kuanza kwa uvamizi wa adui wa Marekani na Kizayuni, idadi ya ndege zisizo na rubani za adui zilizodunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya Jeshi pamoja na IRGC imefikia ndege 82.