Uchokozi wa Marekani dhidi ya Iran unatokana na tamaa ya kupora rasilimali za nishati na kushindana na China
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137264-uchokozi_wa_marekani_dhidi_ya_iran_unatokana_na_tamaa_ya_kupora_rasilimali_za_nishati_na_kushindana_na_china
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ameashiria hatua za uchokozi za Marekani katika sehemu mbalimbali za dunia, ikiwa ni pamoja na shambulio dhidi ya Iran na kusema kuwa hatua zote kama hizo zinatokana na tamaa ya Marekani ya kudhibiti na kupora rasilimali za nishati na kushindana na China.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Mar 10, 2026 06:27 UTC
  • Uchokozi wa Marekani dhidi ya Iran unatokana na tamaa ya kupora rasilimali za nishati na kushindana na China

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ameashiria hatua za uchokozi za Marekani katika sehemu mbalimbali za dunia, ikiwa ni pamoja na shambulio dhidi ya Iran na kusema kuwa hatua zote kama hizo zinatokana na tamaa ya Marekani ya kudhibiti na kupora rasilimali za nishati na kushindana na China.

Esmaeil Baghaei aliandika katika ujumbe kwenye jukwaa la kijamii X (zamani Twitter), akishiriki kiungo cha makala iliyochapishwa na msemaji wa Ikulu ya White House ambayo inaeleza kwa kina sababu kuu ya uchokozi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran , yaani jitihada za kudhibiti rasilimali za mafuta za Iran. Amesema: “Makala hii inaeleza wazi kwamba lengo kuu la uchokozi wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran ni kupata udhibiti wa akiba za mafuta za Iran, ambazo zinachukuliwa kuwa ‘kipande cha mwisho cha fumbo’ katika mkakati mpana wa kutawala usambazaji wa nishati duniani.”

Ameongeza kuwa makala hiyo inaeleza kwamba mara tu udhibiti wa mafuta ya Venezuela na Ghuba ya Uajemi utakapofanikishwa, China haitaweza tena kupata nishati ya bei nafuu, jambo ambalo litadhibiti kupanda kwa uwezo wa kiteknolojia na kiuchumi wa nchi hiyo.

Baghaei ameendelea kusema: “Kama ilivyosisitizwa hapo awali, Iran haijilindi tu dhidi ya vita hivi visivyo na huruma, bali kwa hakika inalinda kanuni za msingi za uhuru wa kitaifa na haki ya kujitawala, mustakabali wa eneo hili, na maslahi ya jumuiya ya kimataifa.”

Ameongeza kuwa hili ni suala la kweli la kimataifa, linalohusiana na dhana za msingi kama vile uhuru, mamlaka ya kitaifa, kuheshimu kanuni za kimataifa, na upatikanaji wa haki wa rasilimali za nishati.

Mwisho, Baghaei amesema kuwa ukweli huu unapaswa kuwafanya wote , majirani wa kieneo, washirika katika Ukanda wa Kusini duniani, mashirika ya kikanda, na watu duniani kote,  kutambua kwamba mapambano yao pia ni mapambano ya wote ni vita vya kulinda mamlaka ya kitaifa, uhuru, haki katika nishati, na mfumo wa kimataifa unaozingatia sheria za kimataifa bila kutawaliwa na sera za mabavu.