Onyo la Larijani kufuatia vitisho hewa vya Trump dhidi ya wananchi wa Iran
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ametoa onyo kali akijibu vitisho vipya vilivyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani vya kuwashambulia na kuwaua wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ali Larijani amesema katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa X leo Jumanne kuwa, taifa la Iran haliogopi vitisho hewa vya maadui, akimuonya Trump kwamba yumkini yeye ndiye atakayetokomezwa.
Dakta Larijani amesema, "Taifa shupavu la Iran, huku likipata ilhamu ya mafundisho ya Ashura, haliogopi vitisho hewa vya Rais wa Marekani."
Akimhutubu Trump, Larijani ameeleza bayana kuwa, "Hata waliokuwa wababe zaidi yako, walishindwa kulitokomeza taifa la Iran. Kuwa makini usije ukatokomezwa wewe."
Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema vitisho hivyo vipya vilivyotolewa na Trump dhidi ya wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ni kukiri wazi wazi kwa kiongozi huyo wa Marekani juu ya kufanya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.
Amesema Iran itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kujilinda kwa mujibu wa Hati ya Umoja wa Mataifa, mpaka pale Baraza la Usalama la UN litakapotekeleza jukumu lake la kuidhaminia dunia amani na usalama.