Rais wa Iran atangaza masharti ya kusitishwa vita vya kutwishwa vya US, Israel
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian ametangaza masharti kadhaa ya kuhitimisha vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu; huku tawala mbili hizo za kigaidi zikiendelea kushambulia maeneo muhimu ya kiraia kama shule, hospitali, makazi ya watu, na turathi za kihistoria za nchi hii.
Katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X, Rais Pezeshkian amesema: Katika mazungumzo yangu na viongozi wa Russia na Pakistan, nimesisitiza kujitolea kwa dhati Iran kwa amani ya eneo.
Dakta Pezeshkian amesisitiza kuwa: Njia pekee ya kuhitimisha vita hivi, vilivyowashwa na utawala wa Kizayuni na Marekani, ni kutambuliwa haki halali za Iran, kulipwa fidia, na kupewa dhamana madhubuti ya kimataifa ya kutovamia tena Iran katika siku zijazo.
Rais wa Iran amesambaza ujumbe huo baada ya kufanya mazungumzo ya simu na Rais Vladimir Putin wa Russia na Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ambapo wamejadili hali ya mambo katika eneo na mahusiano ya pande mbili.
Itakumbukwa kuwa, Marekani na Israel zilianzisha hujuma za kigaidi dhidi ya Iran Jumamosi ya tarehe 28 Februari na kumuua shahidi Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, makamanda kadhaa wa kijeshi, na mamia raia wakiwemo watoto wadogo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa itaendeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Operesheni ya Ahadi ya Kweli 4, ili kuwaadhibu vikali maadui walioanzisha uchokozi.
Jamhuri ya Kiislamu ilikuwa imeonya mara kadhaa kuwa, shambulizi lolote dhidi yake litawasha moto mkubwa katika eneo la Asia Magharibi.