Jeshi Iran lashambulia makao ya Shin Bet na vituo vya ndege za kivita Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137314-jeshi_iran_lashambulia_makao_ya_shin_bet_na_vituo_vya_ndege_za_kivita_israel
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu limetangaza kutekeleza shambulio la droni au ndege ya kivita isiyo na rubani dhidi ya kituo cha kijeshi cha Palmachim pamoja na makao ya Shin Bet ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2026-03-12T06:02:00+00:00 )
Mar 12, 2026 06:02 UTC
  • Jeshi Iran lashambulia makao ya Shin Bet na vituo vya ndege za kivita Israel

Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu limetangaza kutekeleza shambulio la droni au ndege ya kivita isiyo na rubani dhidi ya kituo cha kijeshi cha Palmachim pamoja na makao ya Shin Bet ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu katika taarifa yake ya nambari 24 limesema:

Katika saa zilizopita, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetekeleza mashambulizi kwa kutumia droni za kujitoa mhanga dhidi ya mnara wa ulinzi, barabara ya kurukia ndege na mahala pa kuegeshea ndege katika vituo vya jeshi la anga vya “Palmachim” na “Ovda” vya utawala wa Kizayuni wa Israel pamoja na makao ya shirika la usalama wa ndani la utawala huo, yaani “Shin Bet”.

Kituo cha anga cha Palmachim, kilicho karibu na Tel Aviv, kinahesabiwa kuwa kitovu cha kurusha satelaiti na majaribio ya makombora ya utawala wa Kizayuni wa Israel, na pia ni mahali pa kuwekwa mifumo ya ulinzi wa makombora kama vile “Fimbo ya Daudi (David’s Sling)” pamoja na droni za aina ya Hermes 900.

Kituo cha anga cha Ovda ni miongoni mwa miundombinu ya kimkakati na pia hutumika kama kituo cha mafunzo kwa Jeshi la Anga la utawala wa Kizayuni. Kituo hiki pia kimewahi kutumiwa kuegesha ndege za kivita za Marekani aina ya F‑22.

Shirika la “Shin Bet” linachukuliwa kuwa kitovu cha operesheni za shirika la usalama wa ndani la utawala wa Kizayuni, likiwa na majukumu kama kuongoza operesheni za kiusalama, kuratibu ulinzi wa viongozi muhimu, pamoja na kulinda miundombinu nyeti ya utawala huo.

Vita hivi  vya kulazimishwa, vilivyoanza asubuhi ya tarehe 28 Februari sawa na 10 Ramadhani  kufuatia shambulio la kigaidi la Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vinaendelea huku adhabu dhidi ya wavamizi ikiendelea kubaki katika ajenda kuu ya vikosi vya ulinzi vya Iran.