Rais wa Iran amwambia Macron: US, Israel ndio mzizi wa ukosefu wa usalama katika eneo
Rais wa Iran amesema Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ndizo chimbuko la ukosefu wa usalama na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi, akisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitasita kukabiliana na wavamizi.
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema hayo katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron na kueleza kuwa, wavamizi wangali wanashambulia maeneo muhimu ya Iran ikiwemo miundomsingi ya kiraia, kitendo ambacho amesema kinasikitisha.
Kuhusu hatua ya Marekani ya kushambulia visiwa vitatu vya Abu Musa, Tomb Kubwa na Tomb Ndogo ambavyo ni milki ya Iran, Rais Pezeshkian amesema, mashambulizi dhidi ya meneo hayo muhimu ya Iran yamefanywa kutokea nchi zinazoizunguka Ghuba ya Uajemi.
Dakta Pezeshkian amesisitiza kuwa, kuiruhusu Marekani kuishambulia Iran kutoka katika ardhi za nchi za eneo kunaenda kinyume na sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa.
"Serikali na vikosi vya ulinzi vya nchi hii havifuatilii taharuki wala mgogoro, lakini hatutasita kukabiliana na wavamizi, na kulinda mamlaka ya kujitawala nchi na ardhi yetu," ameeleza Rais wa Iran. Pezeshkian amesisitiza kuwa, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ndio chanzo cha ukosefu wa usalama na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi.
Kadhalika Rais wa Iran amezikosoa baadhi ya nchi za Ulaya kwa kuunga mkono jinai zinazofanywa na Marekani na utawala haramu wa Israel dhidi ya Iran, akiziasa zifungamane na sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Kwa upande wake, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesisitizia udharura wa kusitishwa vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran, huku akielezea wasiwasi wake kuhusu kushadidi hali ya mambo katika eneo, hali ya sasa katika Lango Bahari la Hormuz, na mzozo baina ya Israel na Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon.