Ndege kadhaa za kivita za Marekani zatunguliwa Iran, hadi sasa droni 160 za adui zimedunguliwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137788-ndege_kadhaa_za_kivita_za_marekani_zatunguliwa_iran_hadi_sasa_droni_160_za_adui_zimedunguliwa
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema vitengo vyake vya ulinzi wa anga vimeangamiza ndege kadhaa za kijeshi za Marekani katika “siku nyeusi” kwa majeshi ya nchi hiyo na utawala ghasibu wa Israel.
(last modified 2026-04-04T07:44:03+00:00 )
Apr 04, 2026 07:28 UTC
  • Ndege kadhaa za kivita za Marekani zatunguliwa Iran, hadi sasa droni 160 za adui zimedunguliwa

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema vitengo vyake vya ulinzi wa anga vimeangamiza ndege kadhaa za kijeshi za Marekani katika “siku nyeusi” kwa majeshi ya nchi hiyo na utawala ghasibu wa Israel.

Katika taarifa iliyotolewa mapema Jumamosi, IRGC imesema kikosi chake cha ulinzi wa anga kimetungua ndege ya kivita ya Marekani aina ya F-15 na ndege nyingine ya kivita aina ya A-10 katika anga ya Iran. Taarifa hiyo imesema kikosi hicho pia kimetungua makombora mawili ya  cruise katika anga ya Khomein na Zanjan, droni mbili za kivita za MQ-9 juu ya Isfahan, na ndege moja isiyo na rubani ya Hermes katika anga ya Bushehr kwa kutumia mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga ya jeshi la Iran.

Kwa kupigwa na kutunguliwa droni hizi 3, jumla ya ndege zisizo na rubani za adui zilizotunguliwa na kuharibiwa hadi sasa na mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran zimefikia 160.

Helikopta mbili za za kivita za Marekani aina ya Black Hawk pia zilitunguliwa jana katika anga ya Iran.

Ikiyataja matukio hayo kuwa ni ‘siku nyeusi kwa Jeshi la Anga la Marekani na utawala wa Kizayuni,’ Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesisitiza udharura wa kuzidishwa ufanisi wa uwezo wa ulinzi wa Iran.

Televisheni ya CCN imetangaza kuwa kuangushwa mtawalia ndege za kisasa za kivita za Marekani nchini Iran kunakadhibisha madai ya Donald Trump kwamba Marekani imeangamiza mfumo wa ulinzi wa anga wa Jamhuri ya Kiislamu.