Jeshi la IRGC lashambulia Kamandi ya Jeshi la Marekani na ngome za Israel katika Ghuba ya Uajemi
-
Makombora ya Iran dhidi ya ngome za adui
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetekeleza wimbi jipya la mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani (droni) dhidi ya shabaha mbalimbali zenye mfungamano na Marekani na Israel katika eneo la Ghuba ya Uajemi katika sehemu ya wimbi la 97 la Oparesheni Ahadi ya Kweli-4.
Jeshi la IRGC limesema kuwa kikosi chake cha anga kimefanya oparesheni kubwa mseto kwa kutumia makombora ya balistiki na droni.
Moja kati ya shabaha kuu zilizolengwa katika oparesheni hii tajwa ni eneo walipokuwa wamekutania makamanda na maafisa wa Marekani karibu na kambi ya jeshi ya jeshi la anga ya Mohammed al Ahmad nchini Kuwait.
Kwa mujibu wa IRGC, shambulizi hilo lilipiga kwa usahihi na kusababisha maafa makubwa; ambapo gari nyingi za kubebea wagonjwa zimeonekana katika eneo la tukio baada ya shambulizi.
Taarifa ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia imeongeza kuwa meli yenye mfungamano na Israel kwa jina la King Dao Star imepigwa kwa kombora la kruzi la al Ghadir katika bandari ya Jebel Ali huko Imarati (UAE) ambapo meli iliwaka moto.
Hali ya wasiwasi imeongezeka pakubwa katika miezi ya karibuni kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Tehran kwa upande wake imekuwa ikitumia uwezo wake wa makombora na droni kujibu hujuma za kijeshi za adui.
Iran pia imezuia kupita meli za adui katika Mlango Bahari wa Hormuz ambao kwa makadirio moja ya tano ya mafuta ya dunia nzima hupitia hapo. Mlango Bahari huo aidha ni moja ya korido za kimkakati na nyeti sana za baharini duniani.