Qalibaf: Hakuna mazungumzo chini ya vitisho, Iran iko tayari kufichua kadi mpya uwanjani
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amesema Tehran haitakubali kufanya mazungumzo na Washington chini ya kivuli cha vitisho.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye akaunti yake ya X mapema Jumanne, Qalibaf alimkosoa Rais wa Marekani, Donald Trump, akisema anachukua hatua kwa msingi wa dhana potofu.
Kauli zake zilikuja kufuatia kile Iran inachokieleza kuwa ukiukaji unaoendelea wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa wiki mbili zilizopita. Ukiukaji huo unajumuisha mzingiro wa baharini pamoja na shambulio dhidi ya meli ya kibiashara ya Iran katika Bahari ya Oman siku ya Jumapili.
Spika Qalibaf ambaye kwa sasa ni mkuu wa timu ya mazungumzo amesema: “Trump, kwa kuweka mzingiro wa majini na kukiuka usitishaji wa mapigano, anajaribu, katika dhana yake mwenyewe—kuigeuza meza ya mazungumzo kuwa meza ya kujisalimisha au kutoa kisingizio cha kurejesha uchochezi wa vita.”
Qalibaf amesisitiza kuwa mbinu za mashinikizo hazitakuwa matokeo chanya katika meza ya mazungumzo.
Amesisitiza kuwa: “Hatuwezi kukubali mazungumzo chini ya kivuli cha vitisho,” na kuongeza kuwa, “katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, tumekuwa tukijiandaa kufichua kadi mpya uwanjani.”
Kauli hizo zinakuja wakati duru inayofuata ya mazungumzo kati ya Tehran na Washington imezingirwa na hali ya kutokuwa na uhakika, kufuatia hatua mpya za uchokozi wa Marekani dhidi ya Iran baharini. Hii ilijumuisha tukio ambalo Jeshi la Wanamaji la Marekani limekiuka usitishaji wa mapigano kwa kulenga meli ya kibiashara ya Iran katika Bahari ya Oman.
Jeshi la Iran limesema tukio hilo ni ukiukaji wa taratibu za baharini na kusisitiza kuwa litajibu uchokozi huo.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Marekani, ujumbe wa Marekani ulitarajiwa kusafiri kuelekea Islamabad Jumanne kwa duru inayofuata ya mazungumzo na ujumbe wa Iran.