Iran haina mipango ya kufanya mazungumzo, inalenga kujilinda: Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139916-iran_haina_mipango_ya_kufanya_mazungumzo_inalenga_kujilinda_msemaji_wa_wizara_ya_mambo_ya_nje
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema nchi hiyo haina mpango wa kurudi kwenye mazungumzo na Marekani maadamu Washington inaendelea kukiuka majukumu yake chini ya Mkataba wa Maelewano (MoU) uliosainiwa mwezi uliopita na nchi hizo mbili.
(last modified 2026-07-16T05:55:58+00:00 )
Jul 16, 2026 03:09 UTC
  • Esmaeil Baqaei
    Esmaeil Baqaei

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema nchi hiyo haina mpango wa kurudi kwenye mazungumzo na Marekani maadamu Washington inaendelea kukiuka majukumu yake chini ya Mkataba wa Maelewano (MoU) uliosainiwa mwezi uliopita na nchi hizo mbili.

Esmaeil Baqaei alisema jana Jumatano kwamba Iran kwa sasa inalenga kujibu mapigo na kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya Marekani katika ardhi yake.

"Kwa sasa hatuna mpango wa kufanya mazungumzo na tunalenga kujilinda," Baqaei amesema akijibu madai ya Marekani kwamba mashambulizi yake yanayoendelea dhidi ya Iran yatailazimisha Tehran kurudi kwenye meza ya mazungumzo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Tehran haijitambui kuwa inalazimika kutekeleza tena vipengee vya Mkataba wa Maelewano uliosainiwa na Marekani mnamo Juni 17, akitoa mfano wa ukiukaji wa mara kwa mara wa Washington wa majukumu yake chini ya makubaliano hayo.

"Mkataba wa Maelewano ni seti ya majukumu ya pande zote mbili, na iwapo upande mmoja utakiuka majukumu yake, sisi pia tutaepuka kutimiza majukumu yetu; hii ni kanuni, na njia hii itafuatwa kuanzia sasa," amesema Esmail Baqaei.

Mwanadiplomasia huyo amesema kwamba kila mtu ndani ya Iran anaunga mkono sera ya kusimama kidete dhidi ya Marekani na matakwa yake ya uonevu.

"Majeshi yetu yatajibu kwa nguvu zote kwa mchokozi yeyote. Wakishambulia, watashambuliwa," amesema Baqaei.

Matamshi hayo yamekuja huku Marekani ikiendelea kushambulia maeneo ya pwani kusini mwa Iran, ambapo Washington inadai mashambulizi hayo yanafanywa ili kudhoofisha uwezo wa Iran wa "kulenga meli" katika Lango-Bahari la Hormuz.

Iran imejibu kwa kushambulia vituo na kambi za kijeshi za Marekani katika nchi za Kiarabu za Asia Magharibi kama Kuwait, Bahrain, Jordan na Qatar