Hatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran: Marekani si mchezaji mkuu tena Asia Magharibi
-
Sayyid Abu Torabifard
Imamu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran, amesema Marekani si mchezaji mkuu tena katika eneo la Magharibi mwa Asia, akisisitiza kwamba: "Leo, kwa hatua za Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na mapambano yanayotokana na maarifa na imani ya wapiganaji wa Jeshi la Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefikia kiwango cha juu cha kujilinda ambacho kinamfanya adui asiwezi kuanza chochoko ya aina yoyote bila kupata jibu linalofaa."
Hujjatul Islam Sayyid Muhammad Hassan Abu Torabifard amesema: "Leo tunashuhudia mabadiliko katika mlingano wa vita yanayoashiria nguvu na harakati za kusonga mbele; na hapana shaka kwamba kushambuliwa kambi ya anga ya jeshi la Marekani na Kituo Kikuu cha Amri cha utawala wa nchi hiyo huko Jordan mapema Jumatano ni mojawapo ya ishara za mabadiliko haya."
Amesema kwamba lengo la mkakati mpya ni kuzidisha gharama na hasara ya uchokozi wowote unaowezekana wa adui, na kuongeza: "Ikiwa adui atatambua kwamba gharama ya kuendelea na vita ni kubwa kuliko faida zake, statijia ya kujilinda itakuwa imetimiza lengo lake kuu."
Imamu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amefafanua kwamba: Vita vilivyoanzishwa na Washington na Tel Aviv dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si tu mapambano ya kijeshi, bali ni uwanja wa mapambano na ushindani wa pande zote unaojumuisha vipengele vya kijeshi, usalama, masuala ya kisiasa, kiuchumi, vyombo vya habari, utambuzi, vita vya kisaikolojia na kitamaduni kwa wakati mmoja.
Hujjatul Islam Sayyid Muhammad Hassan Abu Torabifard amesema: "Leo, adui analenga tena majimbo ya kusini mwa Iran kwa mashambulizi ya kioga, na taifa la Iran linashuhudia tena muqawama na kujitolea mhanga kwa watu ambao wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano ya nchi hii katika historia yote."
Katika sehemu nyingine ya hotuba zake za Swala ya Ijumaa, Hujjatul Islam Sayyid Abu Torabifard ametuma salamu makhsusi kwa taifa jasiri la Iraq, waombolezaji wa Arubaini ya Imam Hussein (AS), na washiriki katika shughuli hiyo kubwa.
Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema: "Wanaume, wanawake, vijana, serikali na taifa la Iraq, ambao wamesoma katika shule ya Ashura, kwa miaka mingi wamegeuza ziara ya Arubaini ya Imam Hussein kuwa ishara ya mshikamano miongoni mwa mataifa ya Kiislamu na onyesho la nguvu laini ya muqawama na mapambano."
Sayyid Abu Torabifard ametoa shukrani za dhati kwa watu wa Iraq na wale wanaowahudumia Waislamu wanaozuru Haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) wakati wa ziara ya Arubaini na kusema: "Amani Mungu iwe juu ya watu watukufu wa Iraq na familia zenye heshima za Karbala ambazo zimepata hadhi kubwa ya kuwahudumia wafanyaziara wa Imam Hussein (AS) na mtukufu Abul-Fadhl al-Abbas (AS).
Ameendelea kwa kusema: "Salamu na amani ya Mungu pia iwe juu nguzo imara za muqawama, Hizbullah kwa utashi wake thabiti na imani madhubuti, na salamu ziwaendee wanaume, wanawake na vijana wasiochoka wa Yemen, Gaza na Palestina."