Baqaei: Hakuna mazungumzo na Washington kwa sasa, tunajadiliana na Oman kuhusu njia ya muda Lango-Bahari la Hormuz
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140390-baqaei_hakuna_mazungumzo_na_washington_kwa_sasa_tunajadiliana_na_oman_kuhusu_njia_ya_muda_lango_bahari_la_hormuz
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Hatufanyi mazungumzo na Marekani, na mazungumzo yetu na Oman yanahusu njia ya kupita salama meli katika Lango-Bahari la Hormuz."
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Aug 03, 2026 11:14 UTC
  • Esmaeil Baqaei
    Esmaeil Baqaei

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Hatufanyi mazungumzo na Marekani, na mazungumzo yetu na Oman yanahusu njia ya kupita salama meli katika Lango-Bahari la Hormuz."

Esmaeil Baqaei amesema katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari mapema leo Jumatatu kwamba: "Kwa sasa hatuna mazungumzo ya aina yoyote na Marekani, na mazungumzo yetu na Oman yanalenga katika kuelewana kuhusu njia salama ya kupita meli katika Lango-Bahari la Hormuz."

Ameongeza kuwa: "Lango bahari la Hormuz halikufungwa kutokana na hitilafu za mitazamo kati ya Iran na Oman, bali kutokana na uchokozi wa Marekani tangu tarehe 28 Februari. Maadamu mzingiro wa majini na uovu wa Marekani unaendelea, na vilevile ukiukwaji wake wote wa makubaliano, hakuna mabadiliko yoyote maalumu yatakayoshuhudiwa katika hali ya Lango Bahari la Hormuz."

Matamshi ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran yametolewa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kusema kwamba "Washington inazungumza na Iran kuhusu muundo wa mazungumzo, ambayo yataanza jioni ya leo."

Kuhusu upinzani wa watu wa eneo la Magharibi mwa Asia dhidi ya uwepo wa kijeshi wa Marekani katika eneo hilo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Watu wa eneo hili wanajua kwamba taifa la Iran linapenda amani na linataka kuishi kwa amani na nchi zote katika kanda hii. Wanajua kwamba kila kitu kilichotokea, ikiwa ni pamoja na majibu ya kujihami ya Iran, kililenga chanzo cha uchokozi wa kijeshi, si nchi na watu wa eneo hili. Ni kawaida kwamba wananchi wanapinga uwepo wa majeshi ya Marekani katika nchi zao na hawataki kuona Marekani ikizitumia vibaya nchi hizo."

Akizungumzia mashambulizi yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika nchi za Magharibi mwa Asia, Esmaeil Baqaei amesema: "Uhalifu wa utawala wa Kizayuni unaendelea huko Gaza, Ukingo wa Magharibi na Lebanon. Haya hayafanyiki kwa sababu tu ya hulka ya utawala wa Kizayuni wa Israel, bali pia kwa sababu ya uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo."