Jeshi la Iran laangusha ndege ya kivita ya Marekani ya MQ-9 Reaper katika Lango la Hormuz
-
Jeshi la Iran laangusha ndege ya kivita ya Marekani ya MQ-9 Reaper katika Lango la Hormuz
Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza rasmi kuwa kikosi chake cha anga kimeidungua ndege ya kivita isiyo na rubani ya Marekani aina ya MQ-9 Reaper juu ya Lango la Hormuz, kwa kutumia mfumo wa ulinzi wa anga ulio wa kisasa na wenye uwezo wa hali ya juu.
IRGC ilitoa taarifa hiyo siku ya Jumatatu, ikibainisha kuwa maelezo zaidi kuhusiana na operesheni hiyo ya kijeshi yatatolewa baadaye. Tukio hili, ambalo limethibitishwa na chombo rasmi cha habari cha IRGC cha Sepah News, ni mwendelezo wa pigo kubwa kwa jeshi la Marekani ambalo hutumia ndege hiyo kwa ujasusi na hujuma.
Ndege hiyo ya MQ-9 Reaper, ambayo Jeshi la Anga la Marekani limekuwa ikiiita “zana yenye thamani zaidi” katika kampeni zake za kijeshi dhidi ya Iran, imekumbwa na uharibifu mkubwa tangu vita dhidi ya Iran kuanza mwishoni mwa Februari. Kwa mujibu wa ripoti ya Bloomberg, Iran imeharibu makumi ya ndege za kivita aina ya MQ-9 tangu kuanza kwa vita hivyo vya kigaidi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Kwa gharama ya dola milioni 30 kwa kila ndege, uharibifu wa jumla unakadiriwa kufikia kiasi cha dola bilioni 1.
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya ndege za Reaper zinazofanya kazi katika Jeshi la Anga la Marekani imeshuka hadi kufikia takriban 135, ikiwa chini sana ya kiwango cha chini cha ndege 189 kilichowekwa na jeshi hilo, kulingana na ushahidi uliotolewa bungeni uliotajwa na Bloomberg na The War Zone.
IRGC imerekodi uharibifu wa angalau ndege 41 hadi 42 za MQ-9 Reaper zilizoharibiwa zikiwa katika anga Iran na hata zikiwa ardhini ndani ya kambi za Marekani nchini Kuwait na Jordan.