Baghaei: Mashambulizi ya Marekani dhidi ya maeneo ya raia nchini Iran ni uhalifu wa kivita
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140400-baghaei_mashambulizi_ya_marekani_dhidi_ya_maeneo_ya_raia_nchini_iran_ni_uhalifu_wa_kivita
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema mashambulizi ya Marekani dhidi ya maeneo ya makazi na ya raia katika miji ya Qeshm, Minab, na Lamerd ni uhalifu wa kivita, huku akiahidi kuwa Iran itatumia mifumo yote ya kimataifa inayopatikana kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria.
(last modified 2026-08-04T03:10:12+00:00 )
Aug 04, 2026 03:09 UTC
  • Baghaei: Mashambulizi ya Marekani dhidi ya maeneo ya raia nchini Iran ni uhalifu wa kivita
    Baghaei: Mashambulizi ya Marekani dhidi ya maeneo ya raia nchini Iran ni uhalifu wa kivita

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema mashambulizi ya Marekani dhidi ya maeneo ya makazi na ya raia katika miji ya Qeshm, Minab, na Lamerd ni uhalifu wa kivita, huku akiahidi kuwa Iran itatumia mifumo yote ya kimataifa inayopatikana kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria.

Katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari siku ya Jumatatu, Baghaei alisema kuwa kulenga maeneo ya makazi na tovuti za kiraia kumegeuka kuwa “tabia sugu” ya Marekani.

Ameongeza kuwa Marekani ilianza vita vyake vya kulazimishwa dhidi ya Iran kwa kushambulia maeneo yasiyo ya kijeshi na makazi, akisisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya makazi ya maafisa wa Iran hayana uhalali wowote kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Alisema, “Shambulio dhidi ya makazi ya Kiongozi wetu shahidi [Ayatullah Sayyid Ali Khamenei] na yale ya viongozi wengine mashuhuri halipaswi kutuondoa kwenye uhalisia kwamba vitendo vyote vya Marekani katika kipindi cha miezi mitano iliyopita ni uhalifu wa kivita.” Baghaei ametaja hususan mashambulizi dhidi ya Shule ya Shajareh Tayyebeh huko Minab na uwanja wa michezo wenye watu wengi huko Lamerd, akisisitiza kuwa “yote haya yalikuwa maeneo yasiyo ya kijeshi na ya makazi.” Amebainisha kuwa mashambulizi ya aina hiyo yameendelea katika kipindi chote cha miezi mitano tangu kuanza kwa vita vya uchokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu mnamo Februari 28.

Aidha, ameashiri kukiri wazi maafisa wa Marekani tangu kuanza kwa vita hivyo vya siku 40 kwamba hawatatii vizuizi vya kisheria. Amenukuu matamshi ya waziri wa vita wa Marekani aliyetumia maneno ‘hakuna huruma, hakuna nafasi ya kusalimika’, akisema kauli kama hizo zinaakisi dhamira ya kutenda uhalifu wa kivita. Baghaei amesisitiza, “Kwa hiyo, vitendo ambavyo Marekani imefanya Qeshm, Minab, na Lamerd vyote ni mifano ya uhalifu wa kivita, na nchi zote zina mamlaka na wajibu wa kuwawajibisha wahalifu wa uhalifu huu.”

Shambulio la Februari 28 dhidi ya Shule ya Shajareh Tayyebeh lilitokea siku ya kwanza ya uchokozi wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran na linachukuliwa kuwa shambulio baya zaidi la vita hivi dhidi ya raia. Maafisa wa Iran wamesema idadi ya waliofariki ni 168, wakiwemo wanafunzi 120 na walimu 26. Zaidi ya watu 110 walijeruhiwa. Uchunguzi unaonyesha kuwa makombora matatu ya Tomahawk ya Marekani yaliyolenga shabaha kwa usahihi yalipiga shule hiyo, ambayo ilishambuliwa mara tatu tofauti.