Mshauri wa Kiongozi Muadhamu: Iran iliishinda Marekani katikati ya 'vita vya tatu vya Trump'
-
Meja Jenerali Mohsen Rezaei, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu
Mohsen Rezaei, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesema kuwa Marekani ilishindwa katikati ya "vita vya tatu vya Rais wa Marekani Donald Trump" dhidi ya Iran, huku vikosi vya ulinzi vya Iran vikivuruga mipango ya Marekani, kuilazimisha kuhamisha vituo vyake vya amri na wanajeshi wengi wa nchi hiyo wakiangamizwa na kujeruhiwa; hatua inayozidisha kushindwa kwingine kukubwa katika rekodi ya kufeli ya Marekani.
Akizungumza katika mahojiano maalumu ya televisheni mjini Tehran, Meja Jenerali Mohsen Rezaei aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika kipindi cha 'Kujihami Kutakatifu' ameutaja uchokozi wa karibuni wa Marekani kuwa ni Vita vya Tatu vya Trump dhidi ya Iran, baada ya vita vya awali vya siku 12 na 40.
Mshauri wa Ayatullah Sayyid Mojtaba Husseini Khamenei pia amefichua kuwa, Iran ilijiandaa kushambulia maeneo matatu ndani ya Ukraine ili kujibu shambulio dhidi ya meli yake, lakini ilisitisha operesheni hiyo baada ya Kiev kuomba radhi ikidai kuwa tukio hilo lilijiri kimakosa. Amesema Iran inaendelea kusisitiza kuwa lazima ilipwe fidia ya shambulio dhidi ya meli yake.
"Tulikuwa tayari kushambulia maeneo matatu nchini Ukraine. Lakini baada ya Kiev kudai kuwa shambulio hilo lilifanywa kimakosa tulisitisha hatua yetu ya kulipiza kisasi ili kuchunguza madai yao. Hata kama ilikuwa makosa, lakini fidia iko pale pale," amesema Meja jenerali Mohsen Rezaei.
Katika mahojiano hayo ya televisheni, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ametoa mkono wa pole kwa mnasaba wa maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein (A.S) na kusema: Iran imepiga hatua kubwa katika njia ya kuelekea kwenye ushindi na inapasa kudumisha umoja na uimara wake kwa busara kwa kufuata misingi iliyowekwa na Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Sayyid Ali Khamenei; misingi inayozingatia heshima, hekima na maslahi ya taifa.