Araqchi: Arubaini ya Imam Hussein ni onyesho kubwa la umoja wa kitaifa kati ya Iran na Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140414-araqchi_arubaini_ya_imam_hussein_ni_onyesho_kubwa_la_umoja_wa_kitaifa_kati_ya_iran_na_iraq
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi ameyataja matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein baina ya miji miwili mitakatifu ya Najaf na Karbala nchini Iraq kuwa ni onyesho kubwa la umoja usiovunjika kati ya watu wa Iran na Iraq, akitilia mkazo viunganishi vikubwa vya kidini na kidugu vinavyoendelea kuimarisha uhusiano wa pande mbili.
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Aug 04, 2026 10:35 UTC
  • Abbas Araqchi alifanya ziara ya kila mwaka ya Arubaini ya Imam Hussein (AS) nchini Iraq.
    Abbas Araqchi alifanya ziara ya kila mwaka ya Arubaini ya Imam Hussein (AS) nchini Iraq.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi ameyataja matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein baina ya miji miwili mitakatifu ya Najaf na Karbala nchini Iraq kuwa ni onyesho kubwa la umoja usiovunjika kati ya watu wa Iran na Iraq, akitilia mkazo viunganishi vikubwa vya kidini na kidugu vinavyoendelea kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Katika mahojiano na shirika rasmi la habari la Iraq (INA), Araqchi amesema aliwasili katika mji mtakatifu wa Najaf siku ya Jumatatu na kwamba alikuwa njiani akielekea Karbala kujiunga na ziara ya kila mwaka ya Arubaini ya Imam Hussein (AS), wakati mamilioni ya wafanyaziara wakiendelea kuwasili kwenye maeneo matakatifu nchini Iraq.

"Shughuli hii ni zoezi kubwa linaloonyesha umoja wa mataifa ya Iraq na Iran," amesema Sayyid Abbas Araqchi na kuongeza: "Mazuwari kutoka nchi hizo mbili ndio sehemu kubwa zaidi ya washiriki katika shughuli hii, wakionyesha wazi nguvu ya uhusiano wa kidini na kiitikadi kati ya mataifa yetu mawili."

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amepongeza maandalizi bora aliyoyashuhudia moja kwa moja huko Najaf na kusema: "Nimefuatilia kwa makini mipango bora iliyowekwa ili kuwahudumia wafanyaziara. Kila mtu ameonyesha kuridhika na kiwango cha huduma ikilinganishwa na miaka iliyopita. Hii inaonyesha maendeleo endelevu ya mwaka hadi mwaka katika kuandaa tukio hili zuri."

Araqchi amesisitiza kwamba mshikamano huo wa kina ulionyeshwa waziwazi hapo awali wakati wa mazishi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Sayyid Ali Khamenei katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala, akibainisha wazi kina cha hisia za pamoja na umoja uliokita mizizi kati ya mataifa hayo mawili.

Matamshi hayo yanakuja huku mamilioni ya Waislamu kutoka nchi mbalimbali duniani wakikusanyika katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala kwa ajili ya kumbukumbu ya Arubaini ya Bwana wa Mashahidi na mjukuu mwema wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein bin Ali (AS) wakithibitisha tena ushirikiano wa kimkakati na wa kudumu na uhusiano wa kiroho kati ya Waislamu wa madhehebu na nchi mbalimbali.

Arubaini inaadhimisha siku ya 40 tangu kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussain (AS), Imam wa tatu wa Waislamu na mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), watu wa familia ya Mtume na masahaba wake waaminifu.

Imam Hussein na maswahaba wake waaminifu waliuawa shahidi na utawala wa Yazid bin Muawiya mwaka 61 Hijiria wakipinga utawala dhalimu wa Bani Umayyah uliopotosha mafundisho sahihi ya Mtume Muhammad (SAW) na kueneza dhulma na ufisadi katika jamii. 

Zaidi ya watu milioni 21 walishiriki katika Arubaini ya Hussein (AS) mwaka jana.