Mamilioni ya Wairani washiriki Arubaini ya Imam Hussein, watoa wito wa kulipiza kisasi damu ya Kiongozi aliyeuawa shahidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140416-mamilioni_ya_wairani_washiriki_arubaini_ya_imam_hussein_watoa_wito_wa_kulipiza_kisasi_damu_ya_kiongozi_aliyeuawa_shahidi
Mamilioni ya Wairani wamekusanyika kote nchini kuadhimisha Arubaini ya Imam Hussein bin Ali (AS), ambayo inaashiria siku ya 40 baada ya kuuawa shahidi mjukuu huyo wa Mtume wetu Muhammad (SAW) huko Karbala nchini Iraq mwaka 61 Hijria.
(last modified 2026-08-04T14:54:14+00:00 )
Aug 04, 2026 14:48 UTC
  • Matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (AS), Tehran.
    Matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (AS), Tehran.

Mamilioni ya Wairani wamekusanyika kote nchini kuadhimisha Arubaini ya Imam Hussein bin Ali (AS), ambayo inaashiria siku ya 40 baada ya kuuawa shahidi mjukuu huyo wa Mtume wetu Muhammad (SAW) huko Karbala nchini Iraq mwaka 61 Hijria.

Shughuli za maombolezo na kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein (AS) leo Jumanne imeshuhudia washiriki wakitangaza tena utiifu wao kwa Imam Hussein, huku wakiwaenzi na kutoa heshima maalumu kwa wale waliouawa shahidi na Marekani na Israel katika vita vya sasa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Wakiwa wamebeba bendera nyekundu, washiriki wametoa wito wa kulipiza kisasi kwa damu ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliyeuawa katika shambulia la kushtukiza katika siku ya kwanza ya vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Mkusanyiko mkubwa zaidi ulionekana mjini Tehran, ambapo maandamano ya kila mwaka ya Jamandegane Arbain (kwa maana ya wale walioshindwa kwenda kuzuru kaburi la mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) huko Karbala katika siku ya Arubaini), yalianza kabla ya alfajiri katika Uwanja wa Imam Hussein na yalienea takriban kilomita 15 hadi kwenye kaburi la Hazrat Abdul Adhim al-Hasani katika mji wa Rey, kusini mwa mji mkuu.

Shughuli hiyo, iliyofanyika chini ya kauli mbiu "Simameni kwa Ajili ya Mungu," ilivutia umati mkubwa wa waumini ambao hawakuweza kusafiri kwenda Iraq, na kuunda tena mazingira ya msafara wa Waislamu kutoka Najaf hadi Karbala, ndani ya Iran.

Baadhi ya washiriki katika Arubaini ya Imam Hussein, Tehran

Katika njia yote, washiriki walibeba bendera za Iran pamoja na mabango meusi ya maombolezo na bendera nyekundu zenye maneno "Ya Latharatil-Hussein" yanayohimiza kulipiza kisasi cha damu ya Hussein (as), huku picha za viongozi waliouawa shahidi, mashahidi wa muqawama na wahanga wengine wa vita zikionyeshwa waziwazi.

Waandaaji wameyataja maandamano hayo kuwa yamefanyika kwa ajili ya kumbukumbu ya mashahidi na sisitizo la matakwa ya kulipiza kisasi dhidi ya wale waliohusika na mauaji yao.

Washiriki katika shughuli hiyo wamelitaja tukio hilo kuwa harakati ya kiroho na tamko la uaminifu kwa maadili na malengo ya Ashura ya Imam Hussein (AS).

"Sikuweza kusafiri kwenda Iraq mwaka huu kwa sababu ya afya yangu, lakini sikuweza kukaa nyumbani," amesema Haj Reza, mstaafu mwenye umri wa miaka 68 aliyekuwa akitembea na fimbo na kuongeza: "Miili yetu iko hapa, lakini mioyo yetu inabaki Karbala."

Maryam Sadat, mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 22, amesema maandamano hayo yanawakilisha zaidi ya mkusanyiko wa kidini.

"Ujumbe wetu leo ​​si kutembea tu," amesema Maryam na kuongeza: "Tumekuja kwa ajili ya kumkumbuka Kiongozi wetu aliyeuawa shahidi na mashahidi wengine wa Kambi ya Muqawama ili kuonyesha kwamba shule ya Ashura ya Imam Hussein (AS) inamaanisha kusimama kidete dhidi ya ukandamizaji."

Miongoni mwa washiriki wenye umri mdogo katika shughuli hiyo ya Arubaini ya Imam Hussein mjini Tehran alikuwa Amir Sadra, kijana mwenye umri wa miaka 13 akiwahudumia washiriki kwa vinywaji na sharubati.

Huduma kwa washiriki katika Arubaini ya Imam Hussein (AS), Tehran

"Tumekuwa hapa tangu kabla ya alfajiri," amesema kijana Amir Sadra na kusisitiza: "Kuwahudumia mazuwari wa Imam Hussein ni heshima kubwa zaidi kwetu."

Maandamano kama hayo ya Arubaini ya Imam Hussein (AS) yamefanyika katika miji na maeneo mbalimbali ya Iran kama Mash'had, Tabriz, Karaj na Sari.

Matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (AS) ndio mkusanyiko mkubwa zaidi wa amani wa kila mwaka duniani ambao hukusanya pamoja mamilioni ya watu kutoka nchi tofauti huko Karbala nchini Iraq.