Gharama Halisi ya Vita vya Marekani dhidi ya Iran: Mara Nne ya Makadirio ya Pentagon
Gazeti la Uingereza la The Telegraph limefichua kuwa gharama halisi ya vita vya Marekani dhidi ya Iran ni mara nne zaidi ya kiasi kilichotajwa na Pentagon.
Wakati Wizara ya Vita ya Marekani (Pentagon) imedai kuwa gharama ya vita na Iran ni dola bilioni 37.5, The Telegraph, likiashiria uchambuzi wa Chuo Kikuu cha Harvard, limebainisha kuwa kiasi hicho kinazidi dola bilioni 151. Kiasi hiki kinatofautiana sana na makadirio rasmi ya Pentagon. Gazeti hilo limeangazia ukweli kwamba gharama za muda mrefu za vita hivi hazijazingatiwa.
Kwa mujibu wa ripoti hii, Pete Hegseth, Waziri wa Vita wa Marekani amekadiria gharama ya vita vya Marekani dhidi ya Iran kuwa dola bilioni 37.5 lakini, Linda J. Bilmes, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Harvard na mmoja wa wataalamu wakuu nchini Marekani kuhusu uchumi wa vita, anaelezea makadirio hayo kama "sehemu ndogo tu inayoonekana" ya gharama halisi, akisema kuwa takwimu hiyo haijajumuisha gharama za muda wa kati na mrefu za vita hivyo. Uchambuzi wa gazeti la The Telegraph unaonyesha kuwa iwapo mwenendo wa sasa wa vita utaendelea, jumla ya gharama za vita inaweza kufikia takriban dola bilioni 311.3 kufikia mwisho wa mwaka.
Ni muhimu kuzingatia kuwa takwimu hizi zinahusu tu gharama za kijeshi za vita vya Marekani dhidi ya Iran na hazijumuishi gharama kubwa zinazotokana na sekta nyingine. Madhara ya vita hivi tayari yanaonekana kwa watumiaji wa bidhaa. Bei ya petroli imepanda kwa asilimia 21.7 na bei ya dizeli kwa asilimia 36.7, huku bei ya mafuta ghafi ya Brent ikivuka mara kwa mara kiwango cha dola 100 kwa pipa. Hivyo, Bilmes ameonya kuwa gharama ya mwisho ya hatua hii ya kijeshi dhidi ya Iran inaweza kufikia dola trilioni moja.
Steve Hanke, mhadfhiri wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, pia amebainisha kuwa Rais wa Marekani Donald Trump alianzisha vita vya hiari dhidi ya Iran, ambavyo vitakuwa na gharama kubwa kwa walipa kodi wa Marekani, akisema kuwa gharama ya mgogoro huu itazidi dola trilioni moja. Wakati huo huo, Wizara ya Vita ya Marekani imejaribu kupunguza uzito wa gharama, maafa na uharibifu unaohusishwa na vita dhidi ya Iran ikiwa ni katika juhudi za kupunguza ukosoaji dhidi ya utawala wa Trump. Ingawa Trump aliahidi sera ya "mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi" dhidi ya Iran, lakini matokeo ya vita hivi vya kizembe alivyovianzisha bila sababu ya msingi, ni mkanganyiko wa kiwango cha juu zaidi, machafuko ya kiwango cha juu zaidi na gharama ya maisha ya kiwango cha juu zaidi kwa wananchi wa Marekani.
Takriban mwezi mmoja uliopita, Pentagon ilijulisha Congress ya Marekani kuwa inahitaji takriban dola bilioni 80 za ziada, kiasi kinachozidi makadirio ya awali mara 2.7, ili kugharamia vita dhidi ya Iran. Makadirio hayo kimsingi yalijumuisha silaha mpya, ukarabati wa vifaa na gharama za operesheni pekee bila kujumuisha gharama za kukarabati au kujenga upya vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyoharibiwa na Iran katika eneo. Sababu tofauti zimetolewa kuhusu kutokuwepo uwazi katika ripoti za Pentagon. Kwanza, Pentagon hufanya kazi kwa bajeti finyu, na kuomba kiwango cha juu zaidi kungeongeza mashinikizo kuhusiana na suala la kudhaminiwa fedha hizo. Pete Hegset, aliomba Bunge liidhinishe fedha za ziada, ambapo kuweka wazi gharama kubwa kungefanya kuidhinishwa kwa bajeti hiyo kuwa jambo gumu zaidi.
Kwa upande mwingine, kuficha gharama za muda mrefu huwezesha Pentagon kudhihirisha taswira ya vita inayokubalika zaidi. Gharama kama vile ukarabati wa kambi na matibabu ya majeruhi mara nyingi hazijitokezi hadi miaka kadhaa baadaye, jambo linalofanya gharama hizo kutojulikana kwa umma. Hoja nyingine ni kwamba ripoti za ndani za Pentagon zinakadiria gharama halisi kuwa kati ya dola bilioni 80 na dola bilioni 100, lakini utawala wa Trump unapendelea kutangaza takwimu za chini ili kudumisha uungwaji mkono wa umma kwa vita vinavyoendelea.
Hatimaye, tofauti kubwa kati ya gharama zilizotangazwa na gharama halisi za vita vya Marekani dhidi ya Iran inaonyesha kuwa gharama halisi itakuwa mzigo mkubwa si kwa bajeti ya Pentagon pekee bali pia kwa walipa kodi wa Marekani, gharama ambayo itaendelea kulipwa kwa muda mrefu baada ya vita kumalizika.