Mgawanyiko kati ya Nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi Kuhusu Vita vya Marekani dhidi ya Iran
Kwa mujibu wa gazeti la The Wall Street Journal, nchi za Kiarabu katika eneo la Ghuba ya Uajemi bado zimegawanyika pakubwa kuhusu namna ya kushughulikia vita vya kichokozi na kulazimishwa dhidi ya Iran.
Mgawanyiko mkubwa umejitokeza kati ya nchi hizo kuhusu namna ya kukabiliana na mvutano unaoendelea na Iran. Mgawanyiko huu ni zaidi ya kutokubaliana kidiplomasia tu ambapo unaakisi masuala mahususi ya kiusalama, kiuchumi na kimkakati ya kila nchi katika kukabiliana na mzozo huu ulioanzishwa na Marekani na ambao unatishia usalama na uthabiti wa eneo zima. Katika upande mmoja wa mgawanyiko huu kuna nchi zinazosisitiza ulazima wa kufanyika mazungumzo na kupunguza mvutano, huku upande mwingine ukiwa wa nchi zinazounga mkono msimamo mkali zaidi na matumizi ya mashinikizo ya kijeshi dhidi ya Iran.
Kundi la kwanza linalojumuisha Saudi Arabia, Qatar na Oman, linasisitiza umuhimu wa mazungumzo na hatua za kupunguza mvutano katika kutatua mgogoro uliopo. Mtazamo huu unatokana na uelewa wa wazi wa madhara makubwa ambayo vita vya muda mrefu vinaweza kuusababishia uchumi na usalama wao. Kwa vile uchumi wao unategemea sana mauzo ya nishati na utulivu wa eneo, mataifa haya yana wasiwasi kuhusu kuvurugika kwa njia za usafirishaji wa baharini, kupanda kwa gharama za bima, kukimbia mitaji na kukwama miradi ya maendeleo. Vita vinaziweka nchi hizi katika mstari wa mbele katika mzozo wa kijeshi, ambao zenyewe ndizo zilichangia katika kuuanzisha na kuendelea kwake kwa kuruhusu uwepo wa vituo vya kijeshi vya Marekani katika ardhi zao. Saudi Arabia, ikiwa imerejesha uhusiano wa kidiplomasia na Iran katika kipindi cha utulivu, inaonekana kutotaka kurejea katika hali ya mvutano mkali na Iran licha ya hasira yake kutokana na mashambulizi makali yaliyofanywa na Iran katika kulipiza kisasi cha mashambulizi ya Marekani dhidi yake. Ufalme huo umepinga hata mipango ya kijeshi ya Marekani ya kufungua kwa nguvu Lango Bahari la Hormuz, kwani unaona kuwa maslahi yake ya muda mrefu yanategemea utulivu na uthabiti wa eneo badala ya kuongezeka hatua za kijeshi ambazo zinaweza kuhatarisha malengo yake ya kiuchumi.
Qatar nayo imesisitiza mara kwa mara umuhimu wa suluhisho la kidiplomasia kupitia sera yake ya mambo ya nje inayolenga kutumia upatanishi, ambapo inashirikiana kwa karibu na Oman pamoja na Saudi Arabia kuhusu suala hili. Oman, ikitekeleza jukumu lake la jadi la kupinga mivutano na kuwa mstari wa mbele katika mazungumzo ya kikanda, inaendelea kusisitiza umuhimu wa mazungumzo ili kuhakikisha usalama wa kudumu katika eneo. Nchi hizi tatu zimetambua kuwa mkakati wa kijeshi si tu sio suluhisho lenye tija, bali pia unaweza kuzisababishia nchi za eneo maafa makubwa.
Katika upande wa pili, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Kuwait zimechukua msimamo tofauti na wa uhasama dhidi ya Iran. Kwa kuwa zimeathirika zaidi na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran kupitia makombora na ndege zisizo na rubani, kwa kuungana kikamilifu na Marekani katika uchokozi wake dhidi ya Iran na hata kushiriki katika mashambulizi hayo, nchi hizi zinaamini kuwa Iran haitasitisha vitendo vyake vya kulipiza kisasi bila kuwekewa mashinikizo ya kijeshi na vitisho madhubuti. Hivyo, zimetoa wito kwa Marekani kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya Iran. UAE ambayo yenyewe imetekeleza mashambulizi dhidi ya Iran tangu mgogoro uanze na inahifadhi vituo vya kijeshi vya kigeni, inataka kuunda muungano wa kimataifa ili kufungua tena kwa nguvu Lango-Bahari la Hormuz na imetangaza utayari wake wa kushiriki katika juhudi kama hizo.
Bahrain na Kuwait, zinakabiliwa na hali mbaya zaidi kutokana na kuwa wenyeji wa vituo kadhaa vya kijeshi vya Marekani, na zimeathirika moja kwa moja na mashambulizi ya Iran, ambapo pia ripoti zimeibuka kuhusu ushiriki wao wa moja kwa moja katika vitendo vya kijeshi dhidi ya Iran. Wasiwasi wao mkuu ni kwamba hali inaonyesha kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya vituo vya Marekani katika ardhi zao, inaweza kuhatarisha pakubwa uwekezaji wa kigeni na uchumi wao. Kwa mujibu wa baadhi ya wachambuzi, hitimisho lililofikiwa ni kwamba maelewano yoyote na Iran yataimarisha nafasi yake katika eneo zima la Mashariki ya Kati.
Tofauti hii ya misimamo inatokana na mahesabu tofauti ya kimkakati. Mataifa yanayopendelea mazungumzo na Iran yanaona kuwa utulivu wa muda mrefu utapatikana tu kupitia diplomasia na kwamba gharama za mapambano ya kijeshi zitakuwa kubwa kupita kiasi. Katika upande wa pili, watetezi wa mbinu ya mashinikizo wanasema kwamba kulegeza msimamo mbele ya Iran kutaimarisha tu msimamo wake na kuwatoza gharama kubwa zaidi katika siku zijazo. Kundi hili linafumbia macho nafasi yake ya kuhusika moja kwa moja katika kuibua hali ya sasa, na badala yake kuamua kupiga ngoma ya uadui dhidi ya Iran. Mgawanyiko huu umekwamisha juhudi za kufikiwa msimamo wa pamoja wa Waarabu kuhusu vita vya kichokozi vya Marekani dhidi ya Iran na hivyo kuziweka nchi za eneo katika hali tata. Wakati UAE, Bahrain, na Kuwait zikielekea kwenye ushirikiano mkubwa zaidi wa kiusalama na Marekani, na hata Israel, Saudi Arabia, Qatar na Oman zinafadhilisha kutafuta suluhu kupitia diplomasia huku zikiepuka makabiliano ya moja kwa moja na Iran. Hali hii haijaathiri tu uhusiano wa ndani wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, bali pia imekuwa changamoto kubwa kwa sera za kigeni za Marekani, kwani Washington hutegemea uungwaji mkono wa washirika wake wa Kiarabu kwa hatua yoyote ya kijeshi au kidiplomasia katika eneo.
Inaonekana kuwa mwelekeo wa siku zijazo wa eneo hili unategemea sana ni mbinu gani kati ya hizi mbili yaani kupunguza mvutano au mashinikizo zaidi ya kijeshi, itapata uungwaji mkono zaidi miongoni mwa nchi za Kiarabu na mshirika wao mkuu, Marekani, pamoja na jinsi hali ya mpito kutoka kwenye hali ya sasa ya makabiliano kwenda mfumo mpya wa usalama itakavyoweza kufikiwa. Bila shaka, kuendelezwa msimamo wa uhasama wa Trump na sisitizo lake la kudumisha tishio la kijeshi dhidi ya Iran hakutaleta matokeo mengine yoyote isipokuwa kuzidi kuzorotesha hali ya usalama katika Ghuba ya Uajemi.