IRGC: Watu 8 wenye silaha wenye mfungamano na makundi ya kigaidi watiwa nguvuni kusini-mashariki mwa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140464-irgc_watu_8_wenye_silaha_wenye_mfungamano_na_makundi_ya_kigaidi_watiwa_nguvuni_kusini_mashariki_mwa_iran
Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimetangaza kuwa kimewatia nguvuni watu wanane wenye silaha wenye mfungamano na makundi ya kigaidi katika mkoa wa Sistan na Baluchestan kusini-mashariki mwa Iran kufuatia oparesheni maalum mtawalia.
(last modified 2026-08-06T11:08:40+00:00 )
Aug 06, 2026 11:06 UTC
  • Jeshi la IRGC lawatia mbaroni wahalifu 8
    Jeshi la IRGC lawatia mbaroni wahalifu 8

Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimetangaza kuwa kimewatia nguvuni watu wanane wenye silaha wenye mfungamano na makundi ya kigaidi katika mkoa wa Sistan na Baluchestan kusini-mashariki mwa Iran kufuatia oparesheni maalum mtawalia.

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi, Kituo cha Quds cha Kikosi cha Nchi Kavu cha IRGC kimeeleza kuwa wahalifu hao walikuwa wameunda makundi yenye silaha kwa lengo la kuibua machafuko na ukosefu wa usalama na kufanya hujuma mbalimbali.

Taarifa ya IRGC imeeleza kuwa: Watu hao 8 walihusika katika kuwateka nyara wafanyakazi na wahandisi waliokuwa wakitekeleza miradi ya miundombinu huko Sistan na Baluchestan, walishambulia doria na vituo vya jeshi na vyombo vya kutekeleza sheria, walifanya uporaji wa kutumia silaha na kusambaza hofu katika maeneo ya katikati ya mkoa huo.

Taarifa ya IRGC imeongeza kuwa, watu hao wanane walitambuliwa na kutiwa mbaroni kupitia oparesheni kadhaa maalum za intelijinsia na kwamba silaha mbalimbali zimenaswa kutoka kwa wahalifu hao.

"Wahalifu hao walishirikiana na makundi ya kigaidi kuwateka nyara watu mashuhuri na wahandisi wanaohusika na miradi ya ujenzi na miundombinu katika mkoa wa Sistan na Baluchestan kabla ya kuwakabidhi mateka hao kwa makundi ya kigaidi yanayofanya shughuli zake ng'ambo ya mpaka wa Iran,"imeeleza taarifa ya IRGC.

Vikosi vya usalama vya Iran vimechukua hatua mbalimbali kudumisha usalama na utulivu katika Mkoa wa Sistan na Baluchestan, ambao unapakana na Pakistan na Afghanistan. Katika miaka ya karibuni mkoa huo umekumbwa na mashambulio kadhaa ya kigaidi yaliyowalenga raia na askari usalama.