Iran yayaasa mataifa ya Kiislamu: Ni wakati sasa wa sisi kujitegemea, kuwa na udugu wa kweli
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140498-iran_yayaasa_mataifa_ya_kiislamu_ni_wakati_sasa_wa_sisi_kujitegemea_kuwa_na_udugu_wa_kweli
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa wito wa kuwepo muunganiko na ushirikiano mkubwa wa kikanda, ikitilia mkazo udharura wa mataifa ya eneo kutegemea uwezo wao wa kikanda ili kuondoa uingiliaji wa kigeni.
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Aug 08, 2026 03:24 UTC
  • Iran yayaasa mataifa ya Kiislamu: Ni wakati sasa wa sisi kujitegemea, kuwa na udugu wa kweli

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa wito wa kuwepo muunganiko na ushirikiano mkubwa wa kikanda, ikitilia mkazo udharura wa mataifa ya eneo kutegemea uwezo wao wa kikanda ili kuondoa uingiliaji wa kigeni.

"Waislamu tukisimama pamoja, tunaweza kuzikabili ana kwa ana kila changamoto zinazosababishwa na maajinabi waovu," ameeleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa X.

"Ni wakati sasa wa sisi kujitegemea wenyewe tu, kushikamana na udugu wa kweli," amesisitiza Araghchi katika andiko lake hilo.

Sayyid Abbas Araghchi ametoa kauli hiyo wakati Jamhuri ya Kiislamu inaendelea kutetea muelekeo wa usalama wa kikanda katika Ghuba ya Uajemi, badala ya kutegemea nguvu za kijeshi za nje ya eneo.

Akimalizia andiko lake, Araghchi amevisifu "Vikosi vyenye nguvu vya majeshi ya Iran" kwa "kuonyesha utayari, uwezo, na nguvu za kulikabili jeshi linalotumia gharama kubwa zaidi duniani".

Wakati huohuo Kazem Gharibabadi, naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran wa masuala ya sheria na kimataifa, amesema, utaratibu wa usalama katika Ghuba ya Uajemi ilipasa uanzishwe na nchi zenyewe za eneo hilo, kwa ushiriki wa mataifa yote ya kanda hiyo.

Mwanadiplomasia huyo amesema makubaliano yamepatikana miongoni mwa nchi za mwambao wa kusini mwa Ghuba ya Uajemi kufuatia uchokozi wa kijeshi wa siku 40 ulioanzishwa bila ya sababu na Marekani na Israel dhidi ya Iran na kufuatia kuhitimishwa hati ya maelewano kati ya Iran na Marekani.

Kwa mujibu wa Gharibabadi, imeafikiwa kwamba masuala ya usalama wa kikanda inapasa yajadiliwe na kushughulikiwa na nchi zenyewe za eneo hilo.

Aidha, amesema, makubaliano hayo yaliyofikiwa ni chanya, na kubainisha kuwa Iran imekuwa ikisisitiza kila mara kwamba masuala ya kikanda yanazihusu nchi za eneo hilo na kwamba zenyewe zinapaswa kutekeleza jukumu la kujidhaminia usalama wao…/