Pezeshkian akumbuka mashambulizi ya mabomu ya atomiki huko Hiroshima na Nagasaki, asema mtazamo uleule bado unatawala Washington
-
Rais wa Iran akumbuka mashambulizi ya Hiroshimana Nagasaki
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amelaani mashambulizi ya mabomu ya nyuklia yaliyofanywa na Marekani dhidi ya miji ya Hiroshima na Nagasaki huko Japan na kueleza kuwa mtazamo fikra zilizopelekea kufanyika mashambulizi hayo bado zipo Washington hii leo.
Marekani ilidondosha mabomu ya atomiki huko Hiroshima na Nagasaki tarehe 6 na 9 Agosti mwaka 1945, ikiwa ni mara ya kwanza kwa silaha za nyuklia kutumika vitani duniani.
Kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa, takriban watu 140,000 waliuawa huko Hiroshima, na wengine karibu 74,000 huko Nagasaki. Takwimu hizo zinajumuisha watu walionusurika katika milipuko ya awali lakini baadaye wakafariki dunia kutokana na madhara ya mionzi ya silaha hatari za nyuklia.
"Katika kumbukumbu hiyo ya mashambulizi ya mabomu ya atomiki yaliyofanywa na Marekani dhidi ya watu wa Hiroshima na Nagasaki huko Japan – ambayo ni miongoni mwa jinai kubwa zaidi dhidi ya binadamu- wale wanaopinga ukatili huo wanapasa pia kulaani mtazamo huohuo wa Washington ambao hii leo unatishia kuyafuta mataifa mengine na kuharibu miundombinu ya kiraia," ameandika leo Rais wa Iran kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya X.
Rais Pezeshkian ameeleza haya akikumbusha vitisho vingi vilivyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya Iran, ikiwa ni pamoja na kutishia kuirejesha Iran "kwenye Enzi ya Mawe" na kwamba "ustaarabu mzima utatoweka" kutokana na mashambulizi ya Marekani.
Marekani na Israel zilianzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran tarehe 28 Februari, pale washirika hao wawili walipofanya mashambulizi makubwa katika ardhi ya Iran; hatua iliyoipelekea Tehran kuanzisha wimbi la mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya vituo na kambi za kijeshi za Marekani na Israel katika kanda ya Magharibi mwa Asia.
Iran pia ilifunga Lango-Bahari la Hormuz— njia muhimu ya kimataifa ya usafirishaji wa nishati- kufuatia mashambulizi hayo; hatua iliyozidisha mashinikizo kwa Marekani na washirika wake wa kikanda.