Mshauri wa Kiongozi Mkuu Iran asema vikosi vya Marekani lazima viondoke Asia Magharibi, ahimiza ushirikiano wa kikanda
-
Dkt. Ali Akbar Velayati, Mshauri Mkuu wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu
Mshauri mkuu wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ali Akbar Velayati, amesema vikosi vya majeshi ya kigeni lazima viondoke Asia Magharibi, akitaja uwepo wao wa kama chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama na utulivu katika eneo hilo.
Katika ujumbe wake uliochapishwa kwenye mtandao wa X jana Jumamosi, Dokta Velayati alisema kushindwa Marekani na utawala wa Israel "kumeimarisha imani kwamba vikosi vya majeshi ya kigeni – ambavyo ni chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama - lazima viondoke katika eneo hili."
Amesema matukio ya hivi karibuni "yamechochewa na muqawama wa vikosi vya jeshi, ustahimilivu na uimara wa watu wa Irani, na vilevile ujasiri wa Mhimili wa Muqawama."
Ali Akbar Velayati pia ameeleza kuwa nchi za kikanda zina uwezo wa kulinda usalama wao zenyewe bila kutegemea nguvu za kigeni au uwepo wao wa kijeshi, akihimiza ushirikiano mkubwa ili kudhamini usalama wa kikanda kupitia uratibu wa karibu zaidi.
Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba usalama wa kikanda unapaswa kulindwa na nchi za eneo hilo na kwamba uwepo wa vikosi vya majeshi ya kigeni huchangia katika kukosekana utulivu na usalama.
Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya vituo na kambi za kijeshi za Marekani katika eneo lote Magharibi mwa Asia yameashiria mabadiliko makubwa katika mlingano wa kimkakati katika eneo la Asia Magharibi, na kuangazia zaidi uchunguzi unaoongezeka wa uwepo wa jeshi la Marekani katika eneo hilo.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Jeshi la Iran walifanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya kambi na vituo hivyo katika eneo lote la Ghuba0 ya Uajemi kujibu mashambulizi ya Marekani yaliyoendelea kusini mwa Iran mwezi uliopita.
Mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi yaliwaua wanajeshi wengi wa Marekani, kuharibu ndege za kivita za kisasa na kuashiria kwamba wigo wa kijiografia wa vita vilivyoanzishwa dhidi ya Iran ulikuwa umepanuka zaidi ya matarajio ya awali.
Mbali na athari zake za kijeshi za haraka, mashambulizi hayo pia yameibua mjadala mpya kuhusu uwepo wa vituo vya kijeshi vya Marekani katika nchi mbalimbali za Asia Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jordan, na msimamo wa muda mrefu wa Tehran kwamba usalama wa kikanda unapaswa kusimamiwa na nchi za Asia Magharibi badala ya mataifa ya kigeni.