Kwa nini Trump amekwama katika "fedheha ya kimkakati" katika vita dhidi ya Iran?
Gazeti la Financial Times, huku likinukuu wachambuzi mashuhuri, linaripoti kuwa Trump amekwama katika "fedheha ya kimkakati" kuhusiana na vita dhidi ya Iran na kwamba hawezi kujiondoa katika hali hiyo bila kulipa gharama za kisiasa nchini kwake.
Katika uchambuzi wa kina kuhusu vita vya Marekani dhidi ya Iran, Financial Times linaangazia maana ya "fedheha ya kimkakati", ambapo rais wa Marekani aliyeanzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran kwa kaulimbiu za "kuipindua Jamhuri ya Kiislamu" na kutaka Iran "ijisalimishe bila masharti," sasa anajikuta amenasa katika mtego wa vita ambavyo hawezi kujinasua kwa heshima wala kuviendeleza bila kulipa gharama kubwa za kisiasa ndani ya nchi yake. Katika kipindi cha miezi mitano iliyopita, Trump na washauri wake wamekuwa wakidai mara kwa mara kwamba makubaliano na Iran yanakaribia kufikiwa, lakini hata kama makubaliano kama hayo yatafikiwa kupitia mazungumzo kati ya Iran na Oman, hayawezi kufanikisha malengo ambayo Rais wa Marekani aliyaweka mwanzoni kabisa mwa mzozo wa sasa.
Madai ya awali ya Trump ambayo yalijumuisha makubaliano kuhusu shughuli za nyuklia za Iran, makombora ya masafa marefu (ballistic missiles), na makundi ya muqawama ya kikanda, sasa yamepungua na kubakia kwenye suala moja tu, nalo ni kuitaka Iran iruhusu Lango-Bahari la Hormuz lirejee katika hali yake ya kabla ya vita.
Likiashiria kauli za hivi karibuni za Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, ambaye alisisitiza kuwa kuizuia Iran kuwa taifa lenye nguvu za nyuklia ndilo lengo kuu la makubaliano yoyote, gazeti hilo limemnukuu akisema karibuni: "Makubaliano tunayofuatilia kwa sasa na kwa dharura yanahusu hasa kufunguliwa kwa Lango-bahari la Hormuz." Wachambuzi wanahoji kuwa kauli hizi zenyewe ni ishara ya kudhalilishwa kimkakati Marekani.
Inaonekana kwamba, baada ya miezi mitano ya mapigano, hatamu ya kuendesha mapambano uwanjani imehamia upande wa Iran. Kwa kupanua maeneo ya mapigano kutoka Lango-Bahari la Hormuz hadi Bahari ya Shamu, Iran na 'Mhimili wa Muqawama' (Axis of Resistance) sasa ndio wanaodhibiti kasi na mwelekeo wa vita hivi. Mashambulio ya awali yaliyofanywa na Iran dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Jordan, pamoja na kuongezeka kwa shughuli za 'Mhimili wa Muqawama' katika eneo, yote hayo yanaakisi mkakati mpya wa Iran ambao ni ima kumzuia Trump kuanzisha mashambulio makubwa ya kijeshi dhidi ya Iran au kumdhoofisha kisiasa kupitia vita vya muda mrefu na vya kuchosha. Mabadiliko haya katika uwiano wa nguvu yamemuweka Trump katika hali ambayo, kila mara anapotishia kufanya shambulio kubwa, hatimaye hulazimika kulegeza msimamo na kurudi nyuma.
Sambamba na masuala haya, Trump anakabiliwa na hali tata ndani ya Marekani kwenyewe. Utafiti uliofanywa kwa ajili ya gazeti la Financial Times unaonyesha kuwa asilimia 58 ya wapiga kura waliojiandikisha nchini Marekani wanaamini kuwa vita dhidi ya Iran "havistahili gharama zinazolipwa." Mgogoro wa aina hii bila shaka hautaathiri tu uungaji mkono kwa Trump kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula, Novemba 2026, bali pia utapunguza kwa kiasi kikubwa akiba ya kimkakati ya makombora ya Tomahawk na mifumo ya kuzuia makombora ya THAAD na Patriot.
Trump anaonekana kukabiliwa na hali ngumu katika kuchagua moja ya njia mbili hizi. Kwa upande mmoja, kuchochea vita dhidi ya Iran kunamaanisha kuongezeka kwa idadi ya wahanga na kuzama zaidi katika kinamasi kisicho na mwisho na kwa upande mwingine, kukubali makubaliano kwa masharti ya Iran kutamfanya akabiliwe na ukosoaji pamoja na lawama kali za kushindwa katika makabiliano na Iran, kutoka kwa wapinzani wake wa kisiasa. Hivyo, mzozo na Iran si tu umeitumbukiza Washington katika kinamasi kipya, bali pia umedhoofisha uwezo wa Marekani wa kukabiliana na changamoto kubwa zaidi za kimkakati, ikiwemo mivutano inayoweza kutokea na China.
Ni wazi kuwa Trump amekuwa mhanga wa kaulimbiu kubwa ambazo hakuwa na uwezo wa kuzitekeleza. Sasa anajikuta katika hali ambayo hatua yoyote atakayochukua, iwe ni ya kuendeleza mgogoro au kukubali makubaliano ya amani ya aibu na kufedhehesha, itamtumbukiza katika gharama kubwa za kisiasa. Hii ndiyo "aibu ya kimkakati" iliyotajwa na gazeti la Financial Times, hali ambayo nchi inayodaiwa kuwa 'taifa lenye nguvu kuu' (superpower), imeshindwa kufikia malengo yake na pia imepoteza uwezo wa kujinasua kutoka kwenye kinamasi cha mgogoro iliojitakia yenyewe, kutokana na makosa ya kitathmini na kukosa mkakati madhubuti unaoeleweka.