Zolqadr: Lango-Bahari la Hormuz litaendelea kufungwa hadi pale Marekani itakapobadilisha tabia yake
-
Mohammad Baqer Zolqadr
Afisa wa ngazi ya juu wa usalama wa Iran kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa nchi hiyo haitalegeza vikwazo vya usafirishaji kupitia Lango Bahari la Hormuz hadi pale Marekani itakapobadilisha mwenendo wake mbele ya Tehran.
Mohammad Baqer Zolqadr, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran (SNSC), alisema katika ujumbe wake siku ya Jumamosi kwamba: Sera ya Iran katika kuamiliana na Marekani ni kuepuka makubaliano yoyote ambayo yangekiuka haki ya wananchi wa Iran.
"Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran halitarudi nyuma kamwe, iwe ni vitani au katika mazungumzo," ameeleza Mohammad Baqer Zolqadr, ambaye taasisi yake ndiyo inayofuatilia mzozo wa sasa kati ya Iran na Marekani.
Iran imeweka vizuizi vya usafirishaji kupitia Lango Bahari la Hormuz tangu siku za awali za vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi Februari mwaka huu. Njia hiyo ya maji inakidhi moja ya tano ya mahitaji ya mafuta na theluthi moja ya usambazaji wa mbolea duniani.
Katika ujumbe wake kwa vyombo vya habari vya Iran katika maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Waandishi wa Habari, Mkuu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ametaja masharti sita makuu ambayo Iran inayaona kuwa muhimu kwa ajili ya kufunguliwa tena Lango Bahari la Hormuz.
Masharti hayo ni pamoja na Marekani kujiepusha na vitisho au kuvunjia heshima matukufu ya taifa la Iran, kukomesha kabisa uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kislamu na washirika wake wa kikanda, kuondoa mzingiro wa majini na vikwazo vyote dhidi ya Iran, kuirejeshea mali zake zinazozuiliwa na kulipa fidia kwa uharibifu uliotokana na uchokozi huo.