Baghaei: Utawala wa Kizayuni wa Israel ni tishio kubwa zaidi kwa usalama wa kikanda
-
Esmaeil Baghaei msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
Esmaeil Baghaei msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ni tishio kubwa zaidi kwa utulivu, usalama na ushirikiano miongoni mwa nchi za eneo la Asia Magharibi.
Baghaei amesema hayo leo katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari.
Amesema nchi za eneo hili, kufuatia matukio ya Oktoba miaka mitatu iliyopita, kuanzia mpango wa kikoloni wa kuangamiza Palestina inayokaliwa kwa mabavu, mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza, pamoja na mashambulizi ya utawala ghasibu dhidi ya Lebanon na nchi nyingine za eneo hili, zimezidi kufikia hitimisho kwamba tishio kubwa zaidi kwa utulivu, usalama na ushirikiano wa nchi za Asia Magharibi ni utawala wa Kizayuni.
Ameongeza kuwa mpango wa kile kinachojulikana kama “Israel Kubwa”, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon na Syria, pamoja na vitisho vilivyoelekezwa dhidi ya nchi nyingi za eneo hili, zikiwemo nchi zinazoshiriki katika makubaliano ya Pakistan, Saudi Arabia na Uturuki, vinaendelea kuimarisha mtazamo kwamba nchi za eneo hili haziwezi tena, kama ilivyokuwa hapo awali, kutegemea madai ya Marekani kwamba inazihakikishia usalama wao.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa Marekani yenyewe ni miongoni mwa sababu za ukosefu wa usalama katika eneo la Asia Magharibi.
Baghaei ameendelea kusema kuwa, kama siyo msaada wa pande zote unaotolewa na Marekani kwa utawala wa Kizayuni, pamoja na uungwaji mkono wa kisiasa na kinga ya kiitikadi na propaganda inayotolewa kwa utawala huo, Israel isingeweza kuendeleza uhalifu wake katika eneo hili pasi na kuwajibishwa.
Akizungumzia masharti ya Iran ya kufunguliwa tena Mlango wa Hormuz, amesema kuwa lango hilo halikufungwa kutokana na tofauti za kimtazamo kati ya Iran na Oman.
Amesema sababu ya kufungwa kwa njia hiyo ya majini ni uchokozi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran na matumizi mabaya ya mlango huo.