Jarida la Wall Street: Vita na Iran vimefichua udhaifu wa jeshi la Marekani
-
Jarida la Wall Street: Vita na Iran vimefichua udhaifu wa jeshi la Marekani
Jarida la The Wall Street Journal, katika uchambuzi, limeeleza wasiwasi wake kuhusu kufichuka mapungufu na udhaifu wa jeshi la Marekani katika vita na Iran.
The Wall Street Journal limeandika kuwa: Mashambulizi ya Iran dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani eneo la Asia Magharibi, ikiwa ni pamoja na ya hivi karibuni huko Jordan, yanaonyesha tishio linaloongezeka la makombora na ndege zisizo na rubani za adui.
Gazeti hilo limesema kwamba mashambulizi hayo yameonyesha kwamba Marekani haijajiandaa vya kutosha kulinda kambi zake za nje ya nchi, miundombinu muhimu, na maafisa wake.
Uchambuzi huo unadai kwamba tangu kuanza vita, Iran imefanya mashambulizi zaidi ya 2,000 ya anga, makombora, na ndege zisizo na rubani kote Asia Magharibi na kuharibu kwa uchache maeneo 20 yanayotumiwa na jeshi la Marekani katika nchi 8 tofauti.
Gazeti hilo la Marekani pia linadai kwamba Iran hadi sasa imesababisha hasara ya hadi dola bilioni 13 kwa Marekani kwa upande wa uharibifu wa vifaa na zana pekee.
Kwa nujibu wa Wall Street Journal, kwa jumla, Iran imeharibu kabisa au kutia dosari zaidi ya ndege 42 za kijeshi za Marekani.
Gazeti la New York Times pia limejadili tena suala la kupungua akiba ya silaha za Marekani, likiandika: Miezi mitano ya vita na Iran imepunguza akiba muhimu ya silaha za Marekani hadi kiwango cha chini kabisa. Zaidi ya makombora 1,500 ya Patriot na maelfu ya makombora ya masafa marefu na ya balestiki yametumika katika mzozo huo, na ukarabati wa upungufu huo utachukua kwa uchache miaka miwili.
Uhaba huu, uliokuwepo hata kabla ya vita vya sasa kutokana na himaya ya Washington kwa Ukraine, sasa umekuwa mgogoro kamili ambao umedhoofisha sana uwezo wa Marekani wa kujibu vitisho barani Ulaya na Asia.